Zawadi ya Furaha
“Jina Lake ataitwa Immanueli,… Mungu pamoja nasi.” Kwa kuja kuishi pamoja nasi, Yesu alipaswa kumfunua Mungu kwa wanadamu na kwa malaika. Alikuwa Neno la Mungu—wazo la Mungu lililofanywa kusikika. Katika ombi Lake kwa wanafunzi Wake anasema, ‘Naliwajulisha jina Lako,”—“Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli”—“ili pendo lile ulilonipenda Mimi liwe ndani yao.” Lakini sio tu kwamba ufunuo huu ulidhihirishwa kwa ajili ya watoto Wake wenye asili ya duniani.
Ulimwengu wetu mdogo ni kitabu cha kujifunza cha ulimwengu. Kusudi la ajabu la Mungu la neema, siri ya upendo unaokomboa, ni mada kuu ambayo “malaika hutamani kuitazama,” na litakuwa somo lao kwa vizazi vyote. Waliokombolewa na viumbe watakatifu watapata katika msalaba wa Kristo sayansi yao na wimbo wao. Itaonekana kuwa utukufu ung’aao katika uso wa Yesu ni utukufu wa upendo wa kujitolea nafsi. Katika nuru ya Kalivari itaonekana kuwa sheria ya upendo ya kujikana nafsi ni sheria ya uzima duniani na mbinguni; kwamba upendo ambao “hautafuti mambo yake wenyewe” una chanzo chake katika moyo wa Mungu; na kwamba ndani ya Yule Mmoja aliye mpole na mnyenyekevu kumefunuliwa tabia ya Yeye ambaye hukaa katika mwanga ambao hakuna mwanadamu awezaye kuukaribia.
Hapo mwanzo, Mungu alifunuliwa katika kazi zote za uumbaji. Kristo ndiye aliyezitandaza mbingu, na kuiweka misingi ya dunia. Mkono Wake ndio uliotundika malimwengu katika anga, na kuyavika maua ya kondeni. “Milima waiweka imara kwa nguvu Zako.” “Bahari ni Yake, ndiye aliyeifanya” (Zaburi 65:6; 95:5). Yeye ndiye aliyeijaza dunia kwa uzuri, na hewa kwa wimbo. Na katika vitu vyote vilivyomo duniani, na kwenye hewa, na angani, aliandika ujumbe wa upendo wa Baba.
Sasa dhambi imechafua kazi kamilifu ya Mungu, lakini bado kazi hiyo ya mikono inaendelea kuwepo. Hata sasa viumbe vyote hutangaza utukufu wa ukuu Wake. Hakuna chochote, ukiachilia mbali moyo wa mwanadamu wenye ubinafsi, ambacho huishi kwa nafsi yake yenyewe. Siyo ndege arukaye hewani, wala mnyama atembeaye ardhini, bali kila mmoja hutumikia na kuhudumia aina nyingine ya uhai.
Furaha katika Kutoa
Lakini, tukigeuka toka kwenye vitu vidogo vinavyoonesha ukuu wa Mungu, tunamtazama Mungu kupitia Yesu. Kwa kumtazama Yesu tunaona kwamba anadhihirisha utukufu wa Mungu wetu. “Sifanyi neno kwa nafsi Yangu,” Kristo alisema, “Kama vile Baba aliye hai alivyonituma Mimi, Nami ni hai kwa Baba.” “Wala mimi siutafuti utukufu Wangu” bali utukufu wa Yeye aliyenituma (Yohana 8:28; 6:57; 8:50; 7:18). Katika maneno haya kanuni kuu imeanishwa ambayo ni sheria ya uhai kwa ulimwengu.
Vitu vyote Yesu alivipokea kutoka kwa Mungu, lakini alivipokea ili atoe. Hivyo katika nyua za mbinguni, katika huduma Yake kwa viumbe wote: kupitia Mwana huyu mpendwa, uhai wa Baba huwatiririkia wote; kupitia Mwana wimbi la upendo, kwa njia ya sifa na huduma yenye furaha, hurudi kwenye Chanzo kikuu kuliko vyote. Na hivyo kupitia Kristo mzunguko wa ukarimu hukamilishwa, ukiwakilisha tabia ya Mtoaji mkuu, sheria ya uhai.
Mbinguni penyewe sheria hii ilivunjwa. Dhambi ilianza katika kujipenda nafsi. Lusifa, kerubi afunikaye, alitamani kuwa wa kwanza mbinguni. Alitafuta kujipatia utawala wa viumbe wa mbinguni, kuwavuta mbali kutoka kwa Muumba wao, na kujipatia heshima yao. Hivyo alimwakilisha Mungu vibaya, akimhusisha na tamaa ya kujikweza. Kwa tabia yake ya uovu alitafuta kuitumia ili kumfunika Muumba mwenye upendo. Kwa namna hiyo aliwadanganya malaika. Kwa namna hiyo aliwadanganya wanadamu. Aliwaongoza kulionea mashaka Neno la Mungu, na kutouamini wema Wake. Kwa sababu Mungu ni Mungu mwenye haki na uweza mkuu, Shetani aliwafanya wamtazame kama katili na asiyesamehe. Hivyo aliwavuta wanadamu kuungana naye kwenye uasi dhidi ya Mungu, na usiku wa majonzi ukaingia ulimwenguni.
Dunia ilikuwa giza kwa sababu ya kutokumwelewa Mungu vizuri. Ili vivuli hivi vya majonzi viweze kuondolewa, ili ulimwengu uweze kurudishwa kwa Mungu, nguvu ya Shetani ya udanganyifu ilipaswa ivunjwe. Hili lisingefanyika kwa nguvu. Matumizi ya nguvu ni kinyume na misingi ya serikali ya Mungu; Yeye hupendezwa tu na huduma inayotolewa kwa upendo; na upendo hauwezi kulazimishwa; hauwezi kupatikana kwa kutumia nguvu au mamlaka. Ni kwa njia ya upendo pekee ndipo ambapo upendo huamshwa. Kumjua Mungu ni kumpenda; lazima tabia Yake idhihirishwe kinyume na tabia ya Shetani. Kazi hii ingeweza kufanywa na Mmoja tu katika ulimwengu mzima. Yule pekee aliyejua kimo na kina cha upendo wa Mungu ndiye angeweza kuufanya ujulikane. Katika usiku wenye giza wa ulimwengu, lazima Jua la Haki lichomoze, “lenye kuponya katika mbawa Zake” (Malaki 4:2).
Zawadi Kuu kuliko Zote
Mpango wa ukombozi wetu halikuwa wazo lililojitokeza baadaye bila kutazamiwa, mpango ulioandaliwa baada ya anguko la Adamu. Bali ulikuwa ufunuo wa “siri iliyositirika tangu zamani za milele” (Warumi 16:25). Ulikuwa ufunuo wa kanuni ambazo tangu nyakati zote za umilele zimekuwa msingi wa kiti cha enzi cha Mungu. Tangu mwanzo, Mungu na Kristo walifahamu uasi wa Shetani, na pia walijua anguko la mwanadamu kupitia nguvu ya udanganyifu wa yule mwasi. Mungu hakukusudia kwamba dhambi iweze kutokea, bali aliona uwepo wake hata kabla ya kutokea kwake, na akaandaa njia ya kupambana na hali hii hatari na ya kutisha. Upendo wake kwa ulimwengu ulikuwa mkuu sana, kiasi kwamba alifanya agano ili kumtoa Mwanawe pekee mpendwa, “ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yohana 3:16).
Hili lilikuwa kafara ya hiari. Yesu angeliweza kubaki pamoja na Baba. Angeliweza kubaki na utukufu wa mbinguni, na heshima kuu ya malaika. Bali alichagua kurudisha fimbo utawala mikononi mwa Baba, na kushuka chini kutoka kwenye kiti cha enzi cha ulimwengu, ili aweze kuleta nuru kwa walioingiwa na giza, na uhai kwa wanaoangamia.
Kwa maisha na mauti Yake, amefanikisha hata zaidi ya kurejesha kutoka kwenye uangamivu ulioletwa kwa njia ya dhambi. Lilikuwa lengo la Shetani kuleta utengano wa milele kati ya Mungu na mwanadamu; lakini katika Kristo tunaunganika na Mungu kwa ukaribu zaidi kuliko vile ambavyo tungekuwa iwapo kamwe hatukuanguka dhambini. Katika kuchukua asili yetu, Mwokozi amejifunga Mwenyewe kwa jamii ya wanadamu kwa kifungo ambacho kamwe hakiwezi kuvunjwa. Katika nyakati zote za umilele ameungamanishwa nasi. “Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee” (Yohana 3:16).
Kazi ya ukombozi itakuwa imekamilika. Katika mahali ambapo dhambi ilizidi, neema ya Mungu huzidi sana. Dunia yenyewe, mahali hasa ambapo Shetani hudai kuwa yake, siyo tu kwamba patakombolewa bali pia patatukuzwa. Ulimwengu wetu mdogo, ulio chini ya laana ya dhambi, doa moja jeusi katika umbaji Wake tukufu, utapewa heshima zaidi ya malimwengu mengine yote katika uumbaji wote wa Mungu. Mahali hapa, ambapo Mwana wa Mungu alikaa katika ubinadamu; mahali ambapo Mfalme wa utukufu aliishi na kuteseka na kufa, mahali hapa, atakapofanya mambo yote kuwa mapya, maskani ya Mungu yatakuwa pamoja na wanadamu, “Naye atafanya maskani Yake pamoja nao, nao watakuwa watu Wake. Naye Mungu Mwenyewe atakuwa pamoja nao, [na kuwa Mungu wao].” Na katika kipindi chote cha umilele yote usiokoma kadiri waliokombolewa watakapokuwa wakitembea katika nuru ya Bwana, watamtukuza kwa ajili ya Zawadi Yake isiyoelezeka—Immanueli, “Mungu pamoja nasi.”