Zaidi ya Dini

 

Fikiria ulimwengu ambao mambo, watu, na mawazo yangewasilishwa kama jinsi yalivyo hasa. Hakuna udanganyifu wala lolote la kupotosha. Hili ndilo tatizo la dini leo hii. Katika kipindi kilichopita, kwa kweli dini imekuwa hasa njia ya rushwa na ukatili. Dini imelalamikiwa kuwa chanzo cha serikali mbovu na vita duniani. Wachungaji, makuhani, na viongozi wengine wa dini wametumia vibaya fursa ya mahitaji ya kiroho ya watu kwa faida yao wenyewe. Nchi nyingi zimeharibiwa kabisa kwa sababu ya kundi moja la dini linaloshindana na lingine. Katika sababu zaidi ya moja, mashitaka mengi ambayo yameletwa dhidi ya dini huwa ya kweli. Hali hii ya historia ya dini—au vile inavyoonekana kuwa—ni hakika kabisa kwa mojawapo miongoni mwa taasisi kubwa kabisa ya kiulimwengu ya kidini, ambayo ni Ukristo. Wengi wanalichukia kanisa, lakini wanampenda Yesu. Wengi wana hisia mbaya juu ya suala la ushirika wa kanisa na mfumo wa kidini, lakini wako wazi kumpokea Kristo. Gandhi, kiongozi mashuhuri wa harakati za uhuru nchini India katika karne ya ishirini, wakati fulani alisema, “Nampenda Kristo wenu; Siwapendi Wakristo wenu. Wakristo wenu wanatofautiana kabisa na Kristo wenu.” Kunaonekana kuwepo tofauti kubwa kati ya Kristo na Ukristo. Huenda hata wewe umehisi hivi pia.

Yesu Halisi

Kinyume cha hili ni kwamba Yesu alikuwa mwaminifu sana. Katika mafundisho Yake, alikemea manyanyaso na matendo maovu yaliyofanywa na taasisi za dini. Katika Hubiri Lake la Mlimani, alisema, “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza” (Mathayo 5:17). Yesu alikuja kudhihirisha maana halisi ya dini, “sheria na manabii,” ambayo ilikuwa imepinduliwa na kutumiwa vibaya. Kwa kweli, Maandiko ambayo Yeye mwenyewe aliyahubiri nayo pia yalitabiri kutokea baadaye kwa Ukristo wa uongo, na uliopotoka. Ungelisababisha taabu duniani na kuwatesa wale wote ambao wangepingana na mafundisho yake, ambayo yalimwakilisha Mungu vibaya. “Ungelifanya vita” dhidi ya yeyote asiyekubaliana nayo na kumshinda (Danieli 7:21). Licha ya mateso ya kidini zamani hizo na wakati ujao, Yesu hakutaka kuiangamiza dini, bali kudhihirisha maana yake halisi. Kabla ya kifo Chake msalabani, Yesu aliletwa mbele ya Pilato, mtawala wa Kirumi. Pilato alipomhoji kuhusu kukamatwa Kwake na askari wa Kirumi na viongozi wa Kiyahudi, Yesu alisema, “Ufalme Wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme Wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi Wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme Wangu sio wa hapa” (Yohana 18:36). Yesu alifundisha kuwa dini ya kweli haikuwa juu ya mafanikio ya kiulimwengu wala manufaa binafsi, bali ufalme Wake ulihusu kitu fulani ambacho ni zaidi ya ulimwengu huu. Kile ambacho Yesu alikuja kuonesha ni hali ya kiroho safi na halisi, njia yenye hamasa na pia ya kivitendo ambayo hushughulikia si tu matatizo yetu ya kibinadamu, lakini ambayo pia hutatua zile zinazohusiana na mambo ya Kimbingu. Hivi inawezekanaje Mungu mweza yote, aliye kila mahali na wakati wote, na ajuaye kila kitu, aruhusu mateso? Je, wema hushughulikiaje uovu—kwa kutumia nguvu, au kwa kutumia kitu kinginecho? Ufumbuzi wa Yesu lilikuwa ni jambo ambalo ulimwenguni huu hajawahi kulishuhudiwa kamwe. “Ufalme Wangu sio wa ulimwengu huu.” Hebu fikiria juu ya Ukristo ambao ni mtakatifu na safi. Vipi kama ungefahamu nia ya kweli, mafundisho, tabia, na mawazo halisi ya Yesu Kristo katika namna hasa alivyomaanisha? Hakuna udanganyifu. Hakuna machafuko. Vipi kama kungelikuwa na njia ya kumwelewa Kristo katika unyofu Wake? Vipi kama ungeliweza kuelewa upendo, amani, furaha, na imani kwa kina zaidi kama Yesu mwenye alivyozungumzia na kudhihirisha maishani Mwake. Ingekuwaje kama ungeelewa mafundisho ya Yesu bila kuwa na mtazamo wa kisiasa na tafsiri za kidini ambavyo vimeyachanganya mafundisho Yake kwa karne nyingi? Vipi kama Yesu hakuwa kichaa au mwalimu mwema tu? Vipi kama alikuwa zaidi ya kitu chochote ambacho mwanadamu yeyote angeweza kukifikiria, zaidi ya mtu mwenye hekima? Hapa tunapata kuna maelezo ya mwandishi mmoja kumhusu Yesu huyu halisi: “Yesu alikuwa kielelezo kamilifu wa jinsi tunavyopaswa kuwa. Alikuwa mtunzaji makini kabisa wa sheria ya Baba Yake, hata hivyo alienenda katika uhuru kamili. Alikuwa na hamasa zote za mtu mwenye ari, lakini alikuwa mtulivu, mwenye kiasi na mwenye kujizuia. Alikuwa ameinuliwa juu kupita mambo ya kawaida ya duniani, hata hivyo hakujitenga na jamii. Alikula pamoja na watozaushuru na wadhambi, alicheza pamoja na watoto wadogo, na aliwabeba mikononi Mwake na kuwabariki. Alifadhili sherehe ya harusi kwa uwepo Wake. Alitoa machozi kwenye kaburi la Lazaro. Bidii Yake kamwe haikugeuka kuwa hisia kali wala msimamo Wake kuwa ukaidi wa ubinafsi. Ukarimu Wake kamwe haukuwa na ladha ya udhaifu wala huruma Zake hazikuathiriwa kirahisi na hisia za moyo. Aliunganisha pamoja hali ya utoto ya kutokuwa na hatia na nguvu za utu uzima, aliunganisha uchaji kamili kwa Mungu pamoja na upendo wa dhati kwa mwanadamu. Alikuwa na heshima yenye ushawishi iliyounganika na neema ya unyenyekevu yenye mvuto. Alidhihirisha msimamo thabiti usiyoyumba pamoja na upole… Hatuna mifano sita ya kuifuata, wala mitano; tunao mmoja tu na mfano huo ni Kristo Yesu.”

Zaidi ya Dini

Je! unahitaji kuupata ukweli? Utakuwa ukifanya uamuzi ambao mamilioni ya watu wanahitaji kuufanya, lakini wanaogopa. Utakuwa ukifanya hatua moja kuelekea kwenye kuona, kujua, na hata kuamini katika nafsi safi, tabia, na maisha ya Yesu. Piga hatua hii kwa kusoma kitabu cha pekee chenye maelezo ya kina kuhusu maisha, mafundisho, na unabii wa Yesu: The Desire of Ages (Tumaini la Vizazi Vyote). Kama jinsi ambavyo jina lenyewe hupendekeza, kitabu hiki huonesha kwa nini Yesu huamsha tumaini, badiliko, na moyo wa uchaji.