Unabii wa Kale Wadhihirisha Wakati Ujao

 

Mojawapo miongoni mwa unabii wa kale kabisa ulimwenguni huelezea kuwa sayari yetu inakaribia kushuhudia tukio kubwa la kustaajabisha katika historia ya mwanadamu: mwisho wa falme kama tunavyoufahamu unabii huo. Unabii huu hautaji tarehe maalumu—wala mwaka wala muongo wala hata karne. Hata hivyo, maelezo yake ya historia ya mwanadamu yamekuwa sahihi sana kiasi kwamba hatua ya mwisho—moja pekee iliyobakia kutimia—ni hakika kabisa.

Kisa huanza kwa tukio la kusikitisha la uhamisho wa maelfu ya Wayahudi kutoka nchi yao huko Palestina.* Miongoni mwa mateka ambao Mfalme Nebukadneza aliwachukua kwenda Babeli walikuwa vijana wadogo wanne wa kifalme: Danieli, Shadraka, Meshaki, na Abednego. Katika hali inayoonekana kuwa ya ajabu kwetu, lakini iliyokuwa ya kawaida katika kipindi hicho, Nebukadneza aliwaandikisha vijana hawa wanne katika “Chuo Kikuu cha Babeli” ili wapewe mafunzo ya kuwa washauri wa mfalme.

Ndoto ya Nebukadneza

Muda mfupi baada ya haya, mfalme aliota ndoto. Kwa kweli, ilikuwa ndoto ya kuogofya iliyomsumbua sana, lakini hakuweza kuikumbuka alipoamka asubuhi iliyofuata. Akiwa ameshawishika kuwa ndoto ile ilikuwa muhimu sana, Nebukadneza aliwaita washauri wake na kuwaamuru wamwambie kuhusu kile alichokuwa ameota na maana ya ndoto yake.

“Wenye hekima” hawa wakapinga agizo hili la kustaajabisha. Lakini mfalme akasema, “Ama mniambie ndoto hiyo, la sivyo nitaamuru mwuawe!” Licha ya tishio la kifo, hata hivyo, washauri wa mfalme hawakuweza kupata jibu nzuri.

Wakati huo, Danieli na marafiki zake watatu walikuwa hawakuitwa ikulu ya mfalme pamoja na wale washauri wa mfalme. Hata hivyo, huenda kwa sababu walikuwa ni wenye-hekima-mafunzoni, amri hii iliwahusisha wao. Wakati askari walipokuja kuwakamata, Danieli aliomba apewe muda zaidi. Ombi lake lilikubaliwa, na usiku uleule Mungu alimuonesha Danieli ndoto ile aliyoiota Nebukadneza. (Mungu ndiye aliyekuwa amempatia Mfalme ndoto hiyo). Asubuhi iliyofuata askari akamleta Danieli kwa mfalme.

Danieli aifafanua ndoto

Baada ya taratibu za salamu kumalizika, Danieli akamwambia mfalme ile ndoto aliyokuwa ameiota: “Wewe, Ee Mfalme, uliona, na tazama, sanamu kubwa sana…. Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba; miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo. Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe hilo likaipiga sanamu miguu yake, iliyokuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande. Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vya kupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote” (Danieli 2:31-35).

Kimsingi, mfalme alikuwa na shauku ya kujua maana ya ile ndoto. Maelezo ya mwanzo ya Danieli lazima yalikuwa yamemjaza kiburi: “Wewe, Ee mfalme,… u kichwa kile cha dhahabu.” Lakini maneno yake yanayofuata hayakuwa ya kutia moyo kiasi hicho: “Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe.” Danieli alielezea hayo yote, falme tatu zingefuata baada ya Babeli. Watafsiri wengi wa Biblia wanakubali kuwa falme hizo huwakilisha Uamedi-Uajemi, Uyunani, na Rumi.

Lakini Rumi ilikuwa ya mwisho katika mfululizo wa falme zenye nguvu. Ilipoanguka, masalia yake yakawa mataifa mbalimbali ya Ulaya, Afrika Kaskazini, Mashariki ya Kati ambayo tunayafahamu hadi hivi leo. Uangamivu uliosababishwa na lile jiwe kwenye sanamu huwakilisha uangamivu wa mataifa haya mwisho wa dunia, ambapo baadaye Mungu atausimamisha Ufalme Wake Mwenyewe wa milele.

Nini Kinachoshangaza Sana?

Hapa kuna jambo linalostaajabisha sana kuhusu unabii huu. Danieli aliandika unabii huu takriban mwaka wa 600 KK. Alikuwa anauelewa kuhusu Babeli kwa kuwa aliishi huko, na huenda aliifahamu Uamedi na Uajemi katika kipindi alichoandika unabii huu—ingawa utawala huo haukuiangusha Babeli mpaka miaka kadhaa baadaye. Lakini kibinadamu, hakuna namna yoyote ambayo Danieli angeliweza kutabiri kuinuka na kuanguka kwa Uyunani na Rumi au kuvunjika kwa himaya ya Kirumi. Lakini kila kitabu cha sekondari cha historia ya ulimwengu hushuhudia kuwa ndoto ya Nebukadneza ilitimizwa vilevile hasa kama Danieli alivyomfunulia Mfalme!

Baadhi ya wafafanuzi wa Biblia hudai kuwa Danieli aliiandika ndoto yake takribani miaka mia moja na hamsini tu kabla ya Kristo, badala ya miaka 600 KK., kama anavyodai. Hivyo, wanasema, hakuna lolote la kimwujiza kuhusu maelezo yake ya kihistoria. Lakini hata kama Danieli alikuwa ameandika unabii wake mwaka 150 KK., hakuna namna yoyote ambayo ingemsaidia kufahamu kuhusu kuvunjika kwa himaya ya Kirumi na kuwa mataifa mbalimbali, tukio lililofanyika miaka mia nne baadaye.

Hivyo, ukweli wa kushangaza unatukabili: Nabii aliyeishi zaidi ya miaka elfu mbili na mia tano iliyopita aliangalia mbele katika kipindi cha miaka mingi baadaye na kutupatia maelezo sahihi kabisa ya matukio ya siku zijazo.

Hatuwezi kufanya hitimisho lingine lolote kutokana na hoja hii zaidi ya kusema kuwa Danieli aliyapokea maelezo haya ya matukio ya siku zijazo kutoka kwa Mungu Mwenyewe. Na kwa sababu kila kitu katika maelezo ya Danieli juu ya historia ya ulimwengu kimetimizwa, tunaweza kuwa na hakika kuwa tukio la mwisho—mwisho wa dunia kama tunavyoufahamu na kuanzishwa kwa ufalme wa Mungu Mwenyewe—litatokea pia.

*Danieli sura ya 2 huelezea unabii huu. Danieli sura ya 1 huelezea utangulizi wa matukio haya.