Tumaini Baada ya Kifo

 

Kifo cha ghafla cha Michael Jackson mnamo Juni 25, 2009 kiliushtua ulimwengu. Katika huduma ya kumbukumbu ya kifo chake mnamo Julai 7 huko Los Angeles, mwigizaji wa kike aitwaye Brook Shields alijaribu kuwafariji mashabiki wa mwanamuziki huyu mashuhuri waliokuwa wakiomboleza aliposema, “twapaswa kutazama juu kule aliko bila mashaka yoyote kuwa kakaa kwenye mwezi.”

Hivi kweli Michael Jackson alikwenda wapi? Je, mtu fulani huenda wapi anapokufa? Hivi watakatifu mara tu wanapokufa huruka na kupaa kwenda mbinguni, huku wadhambi waliopotea wakitumbukia kuzimu? Hivi kuna mahali paitwapo pagatori au toharani ambapo watu husubiria wakiwa kwenye mateso? Je, tunageuka kuwa mizimu? Vipi kuhusu fundisho kwamba mtu anapokufa anaweza kurudi tena kwa sura ya mtu mwingine au hata kama mnyama fulani, lina ukweli wowote? Je, tunaweza kurudi tukiwa kama panya?

Dunia yetu imejawa nadharia zinazotatanisha, lakini tutafuatilia katika chanzo kimoja pekee: Biblia Takatifu. Kitabu cha mwisho cha Biblia, “Ufunuo,” huonya kwa dhati kwamba malaika aliyeasi aitwaye Shetani “huudanganya ulimwengu wote” (Ufunuo 12:9). Kama jambo hili ni kweli, hatuwezi kutarajia idadi kubwa ya wanadamu kuwa sahihi katika jambo lolote, hasahasa kwenye jambo muhimu kama hili linalohusiana na kile ambacho humtokea mtu aliyekufa baada ya mazishi kuisha.

Mitazamo Mitatu ya Msingi

Hebu tuanze kwa kurahisisha mambo. Kwanza kabisa, kuna mitazamo mitatu ya msingi kuhusu kifo ambayo kwayo mawazo mengine mengi hujitokezea.

Umekufa na Huo Ndio Mwisho Wako—Nadharia hii ya kwanza inafahamika kiasi fulani—ingawa haina tumaini—na huhamasishwa na wale waaminio kwamba uhalisia wote unaweza kueleweka tu kutokana na kile sayansi iwezacho kuelezea. Kwa kutumia msingi wa dhana kwamba “ukionacho ndicho upatacho,” wanaamini kuwa kifo ndio mwisho wa mambo yote. Tunakufa, tunaoza ardhini, tunakuwa chakula cha funza, na hivyo ndivyo ilivyo. Umetoweka.

Roho Isiyokufa—Mtazamo huu wa pili, ambao unafahamika zaidi kuliko zote, hufundisha kwamba tunapokufa ni mwili tu ndio unaooza, wakati Nafsi ya Juu Zaidi au “roho,” huendelea na safari, kama vile nyoka anavyovua gamba lake la juu la ngozi. Kwa kweli dini mbalimbali mara nyingi hutofautiana kila moja na nyingine kuhusu wapi roho zinapoenda baada ya kifo, lakini wazo la msingi la roho kuendelea kuishi baada mwili kufa huaminiwa na watu wengi zaidi.

Roho Zinazokufa na Ufufuo—Mtazamo wa mwisho hudai kuwa neno “roho” humaanisha mtu kamili, na sio kiasili tofauti kinachoweza kujitenga ambacho huendelea kuishi baada ya mwili kufa. Mungu alipomwumba Adamu, “akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai” (Mwanzo 2:7, msisitizo umeongezewa). Kwa hiyo mwanadamu hana roho, bali, badala yake, yeye ni roho. Baada ya mwanadamu kutenda dhambi, nafsi yake yote, au roho, ikawa na ukomo, au ikakabiliana na mauti. Wadhambi wanapokufa, hurudi mavumbini, na “pumzi ya uhai” humrudia Mungu. “Pumzi” hii sio mzimu unaoweza kutembelea sehemu nyingine baada ya mwili wa mtu husika kuzikwa sehemu nyingine, bali badala yake ni nguvu au kanuni ya uhai ambayo iko ndani ya kila kitu hai. Kulingana na mtazamo huu, wakati wa mauti mtu hufa kabisa, yaani, hawajitambui, wamenyamaza, wamelala kaburini, wakisubiri Siku ya Ufufuo.

Mtazamo upi ni sahihi? Kwanza kabisa, tunakataa mtazamo wa kwanza kwa sababu tunaamini kuwa Mungu yupo na kwamba Neno Lake husema kweli. Mbingu ipo, na jehanamu pia ipo. Vipi kuhusu hiyo mitazamo mingine miwili, pamoja na mawazo yake yanayokinzana kuhusu asili ya roho? Je, Kitabu cha Mungu hufundisha nini hasa?

Ukweli wa Biblia kuhusu Kifo

Kama ambavyo tumekwisha kuona, Biblia Takatifu hufundisha hapo kwanza Mungu alipomwumba Adamu, kwamba “akawa nafsi hai” (Mwanzo 2:7). Miaka mingi baadaye, “nafsi sabini” zilikwenda Misri (angalia Kutoka 1:5). Muktadha huonesha kuwa fungu hili halikuwa linazungumzia mizimu sabini, bali wanadamu hai sabini waliokwenda Misri. Je, unaelewa? Nafsi ni mtu.

Ukweli mwingine: wanadamu walioanguka dhambini hawaishi milele. Kama ukiliangalia kwa makini neno “kutokufa” au “kutopatikana na mauti” katika itifaki yoyote ya Biblia, utagundua kuwa inahusika na Mungu tu, kwa sasa. Mungu “peke Yake [ndiye] hapatikani na mauti” (1 Timotheo 6:16), na ni mpaka tu baada ya watakatifu Wake watakapokuwa wamefufuliwa wakati wa kuja kwa Yesu Mara ya Pili ndipo “mwili huu wa kufa” “utapovaa kutokufa” (1 Wakorintho 15:54). Ni dhahiri, watakatifu wa Mungu wasingeweza kuja “kuvikwa” hali ya kutokufa kama wangekuwa nayo hapo awali.

Wazo Lingine: katika Biblia, kifo huitwa “usingizi.” Katika nyakati za Agano la Kale, Mfalme Daudi aliomba ulinzi ili asije “[akalala] usingizi wa mauti” (Zaburi 13:3). Wakati wa mwisho wa dunia, wale wote “walalao katika mavumbi ya nchi wataamka” (Danieli 12:2). Hivyo wafu hulala usingizi kwa amani “katika mavumbi ya nchi” mpaka Siku ya Ufufuo.

Sasa, huu hapa ukweli muhimu. Biblia iko wazi kwamba “wafu hawajui neno lolote” (Mhubiri 9:5). “Hawajui neno lolote” humaanisha kutojua lolote. Sifuri. Mafungu matano yanayofuata baadaye Sulemani hufafanua kuwa “Hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako” (Mhubiri 9:10). Daudi hulirudia jambo hili pale anapoandika, “Sio wafu wamsifuo Bwana, Wala wowote washukao kwenye kimya” (Zaburi 115:17). Kwa hiyo wafu hulala kimya. Hawako huko juu mbinguni wakimsifu Mungu wala hawako hapa chini wakilia. Wala hawawezi kubisha hodi mlangoni kwako baada ya mazishi yao. Kwa maneno mengine, Michael Jackson hachezi tena dansi yake maarufu “akitembea mwezini” mahali fulani ulimwenguni sasa hivi. Badala yake, amekufa, yuko kaburini akisubiri ile Siku ya Hukumu (Waebrania 9:27).

Mfano bora katika Biblia yote ni kuhusu kile kilichotokea kwa Yesu Kristo karibu miaka elfu mbili iliyopita. Katika kipindi cha huduma Yake takatifu, Bwana wetu alitabiri waziwazi kwamba “[angeuawa], na siku ya tatu kufufuka” (Mathayo 16:21). Na hili ndilo hasa lililotokea. Muda mfupi baadaye mikono isiyo miovu ikamkamata, na kumsulubisha. Paulo anafafanua kilichotokea hasa kwamba “Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu” (1 Wakorintho 15:3). Maneno, “Kristo alikufa” humaanisha kuwa alikuwa amekufa kabisa. Siku tatu baadaye malaika mtakatifu akatangaza: “Amefufuka katika wafu” (Mathayo 28:7). Haleluya!

Ni kwa sababu ya ufufuo wa Yesu ndiyo maana tunapata tumaini. Moja ya siku hizi—na itafika mapema kuliko watu wengi wanavyofikiria—Mwokozi wetu atarudi duniani “pamoja na nguvu na utukufu mwingi” akiwa na jeshi kubwa la malaika (angalia Mathayo 24:30-31); na atakapokuja, Paulo anasema ni katika wakati huo ndipo “nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza” na kwamba “tutakuwa pamoja na Bwana milele” (1 Wathesalonike 4:16-17). Hivyo wanaomwamini Yesu watafufuliwa ili kuwa “pamoja na Bwana” atakaporudi mara ya pili.

Hitimisho

Ukweli muhimu ni huu: sote tunafahamu kuwa kifo ni hakika, na huumiza. Hata hivyo, katikati ya majonzi na upotevu, Habari Njema ni kuwa Yesu Kristo anatupenda, amelipa adhabu ya dhambi zetu, akaingia ndani ya kaburi la baridi, na kisha akafufuka na kuwa hai tena, hivyo akashinda kifo na kaburi. Kama tukiuamini ushindi Wake, sisi pia tunaweza kushinda kifo. Muda mrefu uliopita Yesu aliwaahidi wale wanaoitikia na kuukubali upendo Wake, na kuziungama dhambi zao, na kuitumainia neema Yake, kwa kusema: “Nami nitamfufua siku ya mwisho” (Yohana 6:44). Ahadi Yake ni kwa ajili yako leo.