Mwaka 2012 na Mwisho wa Dunia

 

Ilikadiriwa kuwa ifikapo mnamo mwaka 2012, joto kwenye kitovu cha Dunia lingeongezeka kwa kiwango kikubwa ikiwa ni matokeo ya tufani kubwa sana kwenye jua. Hii ingesababisha matetemeko makubwa sana duniani kote. Matetemeko haya yangeibua mawimbi makubwa sana ya maji ambayo yangesababisha uharibifu mkubwa kadri yanavyoelekea nchi kavu. Uharibifu huu mkubwa duniani kote ulioneshwa hivi karibuni kwenye filamu iitwayo “2012”, lakini, je, kuna ukweli wowote juu ya hilo? Je, mambo yote hayo yangetokea mwishoni mwa ile inayojulikana kama “Kalenda Ndefu ya Kuhesabia,” mnamo terehe 21 Desemba, 2012?

Jibu la Biblia ni Hapana. Akizungumzia kurudi Kwake na mwisho wa dunia, Yesu aliwaambia wasikilizaji Wake kwa ujasiri, “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke Yake” (Mathayo 24:36). Asingeweza kueleweka zaidi ya hapa. Dunia itafikia mwisho na Yesu atarudi kwa wakati Wake—na kalenda ya wakati Wake ndiye pekee anayeijua.

Na hata hivyo hatujaachwa kukisia ukaribu wa mwisho wa dunia. Yesu alisema kuwa “[Tutasikia] habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu” (Mathayo 24:6-8). Kutakuwa na majanga mengi zaidi na zaidi duniani katika mazingira tuyaishiyo, kadri ambavyo kuja kwa Yesu kunakaribia, lakini hatakuja mpaka habari njema ya ufalme itakapohubiriwa katika “ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja” (Mathayo 24:14). Kama sauti kubwa ya kengele, taarifa za habari za kila siku kwenye magazeti na TV hutukumbusha juu ya ulimwengu unaosambaratika. Na si watu wachache wanaozungumzia uangamivu wetu usioepukika. Lakini katika rehema Yake kuu, Mungu anasubiri kwa sababu hapendi hata mmoja mingoni mwa watoto Wake apotee. Hata sasa, habari njema ya wokovu zinahubiriwa kwa kasi kote katika sayari hii, zikiwaandaa watu kwa ajili ya ujio Wake.

Lakini swali linabakia. Endapo hatujui wakati sahihi wa kurudi kwa Kristo ni jambo gani, basi, tunalopaswa kufahamu? Swali hili muhimu sana lilijibiwa na Yesu mwenyewe karibu miaka 2,000 iliyopita. Alipokuwa anaondoka duniani hapa, mara baada ya ufufuo, aliwashangaza wanafunzi Wake walipomtazama akichukuliwa mawinguni, akitoweka machoni pao. Lakini karibu Naye kulikuwa na malaika wawili wa mbinguni waliowaeleza ahadi ya kuvutia wafuasi hao wenye huzuni. “‘Enyi watu wa Galilaya,’ walisema, ‘mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda Zake mbinguni’” (Matendo 1:11).

Zingatia kuwa ahadi hii inaendana kabisa na maelezo ya awali ya Kristo kuhusu kurudi Kwake. Kwa msisitizo mkubwa alielezea kweli ili kuondoa dhana zozote za siri kuhusu ujio Wake. Aliwaonya wanafunzi Wake, “Mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule…. Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja Kwake Mwana wa Adamu” (Mathayo 24:23-27).

Mbali na kuwa tukio la siri, kuja kwa Yesu Mara ya Pili kutakuwa ni tukio ambalo kila mtu atalishuhudia. “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. (1 Wathesalonike 4:16). “Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona” (Ufunuo 1:7). Macho yote yatakuwa yanatazama tukio hili kubwa na litakalosikika kila mahali—hakutakuwa na haja ya kutumia Facebook au redio ili kufahamu taarifa hizi. Maelezo haya ya kina ya kurudi kwa Kristo mara ya pili ni muhimu kwa sababu 2 Wathesalonike 2:9 inaonesha kwamba Shetani mwenyewe, kiumbe mwenye mng’ao wa nuru, atajaribu kuudanganya ulimwengu kupitia ujio wa pili wa uongo. Unaweza kusoma zaidi kuhusu mada hii kwenye kitabu kiitwacho, “The Great Controversy” kwenye tovuti ya www.glowonline.org au kwa kutafuta nakala ya kitabu cha Pambano Kuu.

Lakini hii ina maana gani kwako? Hata hivyo, ukweli una faida gani kwako endapo hauko tayari kwa tukio hilo? Ili kuelewa maana ya kuwa tayari ni lazima utambue kuwa Ujio wa Pili unaweza kuwa habari njema! Hakuna sababu ya kuogopa mwisho wa dunia kama uko upande wa Kristo. Ufunuo 6:14-17 huelezea jinsi watu watakavyokimbia kwa hofu na watakavyoangamizwa wakati Kristo atakaporejea mara ya pili kwa sababu wamechagua kuuchukia ukweli wa dhati kuhusu hali yao ya dhambi na kupenda uongo wa kufariji usio wa Kibiblia unaowaambia kuwa wataokolewa katika dhambi zao. Mungu anatamka, “Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu?… Mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi” (Ezekieli 18:23,32). Wakati ulimwengu utakapofikia mwisho na waovu watapokuwa wanaangamizwa, Bwana atakuwa anawapatia kile tu wanachokitaka. Mithali 8:36 inasema “…anikosaye [Mimi Mungu] hujidhuru nafsi yake mwenyewe, na wao wanichukiao hupenda mauti.”

Ili tuwe tayari kwa ajili ya mwisho wa dunia na kurudi kwa Kristo, lazima kwanza tuelewe hali yetu halisi. Biblia inafundisha kwamba mzizi wa dhambi zote ni ubinafsi. Watu wengi hufikiri kwamba wao ni wema, lakini mtazamo wa uaminifu wa Neno la Mungu hudhihirisha kinyume chake. Hata matendo yetu ya fadhila yanaweza kutendwa kwa malengo ya ubinafsi. Tunachohitaji, kwanza, ni msamaha wa Kristo; na pili, moyo mpya wenye upendo usio na ubinafsi. Msamaha huu unaweza kupatikana tu kwa kumwomba Yesu atupatie kwa njia ya sala. Tunapokea moyo mpya na Roho mpya kwa kumtafuta Mungu katika Neno Lake: “Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa Neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele” (1 Petro 1:23).

Kristo anatamani wote tuwe pamoja Naye kwenye ufalme Wake atakaporudi. “Bwana hakawii kuitimiza ahadi Yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikilie toba” (2 Petro 3:9). Kwa kweli Biblia hufundisha kuwa wakati atakaporudi, rafiki zetu na wapendwa wetu waliolala katika Yesu watafufuliwa kwa ajili ya uzima wa milele! “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni… nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo” (1 Wathesalonike 4:16–18).

Ile “Kalenda Ndefu” ya jamii ya watu waliojulikana kama Maya—pamoja na maelezo yake yenye ufasaha kuhusu nafasi za sayari na nyota kwa kipindi cha zaidi ya miaka 5000—ni mafanikio ya binadamu yenye kustajaabisha. Lakini Biblia hutuambia kuwa Mungu ameziweka sayari na nyota kwenye njia zake, na hivyo huongoza miendo yake—na wala sayari na nyota haziongozi mwendo wa Mungu. Ikiwa tuko salama katika Yesu, tusingelikuwa na haja ya kuogopa kuhusu kilichotabiriwa kwamba kingetupata tarehe 21 Desemba, 2012, au siku nyingine yoyote.