Kuzungumza na Mungu

Maombi ni kumfungulia Mungu moyo kama rafiki. Si tu kwamba ni lazima ili kumjulisha Mungu vile tulivyo, bali hutuwezesha sisi kumpokea Yeye. Maombi hayamshushi Mungu chini, bali hutuinua juu aliko Yeye. Wakati Yesu alipokuwa duniani, aliwafundisha wanafunzi Wake jinsi ya kuomba. Aliwaelekeza kupeleka mahitaji yao ya kila siku mbele ya Mungu, na kumtwisha Yeye shida zao zote. Uhakika aliowapatia kwamba maombi yao yatasikiwa, pia ni uhakika kwetu.

Hitaji Letu la Kuomba

Yesu mwenyewe alipokuwa akiishi pamoja na wanadamu, alikuwa kwenye maombi mara kwa mara. Mwokozi wetu alijihusianisha na mahitaji na mapungufu yetu na udhaifu wetu, kwa kuwa alikuwa mwombaji, mtoadua, akitafuta toka kwa Baba Yake kupewa nguvu mpya, ili aweze kuwa tayari kwa kazi na majaribu. Yeye ndiye mfano wetu katika mambo yote. Yeye ni ndugu katika udhaifu wetu, “alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote;” lakini akiwa hana dhambi asili Yake ilipingana na uovu; alivumilia mahangaiko na mateso ya roho katika ulimwengu wa dhambi. Ubinadamu Wake uliyafanya maombi kuwa suala muhimu na fursa ya upendeleo. Alipata faraja na furaha katika kufanya ushirika na Baba Yake. Na kama Mwokozi wa wanadamu, Mwana wa Mungu, aliona haja ya maombi, ni kwa kiasi gani zaidi wanadamu wadhambi na wenye ukomo na dhaifu wanapaswa kuhisi hitaji la dhati la maombi ya kudumu.

Baba yetu wa Mbinguni anangoja kutukirimia baraka Zake tele. Ni haki yetu kunywa kwa wingi kutoka kwenye chemchemi ya upendo usio na mipaka. Ni jambo la kushangaza kiasi gani kwamba tunaomba kidogo sana! Mungu yuko tayari na hupenda kusikiliza maombi ya dhati ya wale walio wanyonge kabisa miongoni mwa watoto Wake, lakini badala yake kuna hali ya kusita sana kwa upande wetu katika kumjulisha Mungu mahitaji yetu. Je, malaika wa mbinguni huwafikiriaje hawa wanadamu maskini, wasio na msaada, wanaokabiliwa na majaribu, wakati ambapo moyo wa Mungu wenye upendo usio na kikomo unatamani sana kuwa karibu nao, ukiwa tayari kuwapatia zaidi ya kile wanachoweza kuomba au kufikiria, lakini bado wanaomba kidogo sana na wana imani ndogo sana? Malaika wanapenda kusujudu mbele ya Mungu; wanapenda kuwa karibu Yake. Wanauchukulia ushirika wao na Mungu kama furaha yao kuu; na bado watoto wa duniani, wanaohitaji sana msaada ambao Mungu pekee anaweza kuutoa, wanaonekana kuridhika kutembea bila nuru ya Roho Wake na ushirika wa uwepo Wake.

Ufunguo wa Ushindi

Giza la yule mwovu huwazunguka wote wanaopuuza kuomba. Minong’ono ya majaribu ya yule adui huwashawishi kutenda dhambi; na hii yote ni kwa sababu hawatumii fadhila yao ambayo Mungu amewapatia katika fursa ya maombi aliyoiteua. Kwa nini wana na mabinti wa Mungu wapuuzie kuomba, wakati maombi ni ufunguo katika mikono ya imani unaofungua hazina ya mbinguni, mahali palipohifadhiwa rasilimali tele za Mungu Mwenyezi? Pasipo maombi yasiyokoma na kukesha kwa bidii tupo katika hatari ya kuzembea na kupotoka kwa kuiacha njia ya kweli. Yule adui daima hutafuta kuweka vizuizi katika njia ya kiti cha rehema, ili kwa kukosa maombi ya bidii na imani tusipokee neema na nguvu ya kuyakabili majaribu.

Omba ukiwa faraghani, peke yako, na kadri unapokuwa ukifanya kazi zako za kila siku hebu moyo wako uinuliwe mara kwa mara kwa Mungu. Hivyo ndivyo Henoko alivyoweza kutembea pamoja na Mungu. Maombi haya ya kimya hupanda juu kama manukato ya thamani mbele ya kiti cha neema. Shetani hawezi kumshinda mtu yule ambaye moyo wake umetulizwa kwa Mungu.

Masharti ya Maombi

Kuna masharti maalumu ambayo kwayo twaweza kutegemea kuwa Mungu atasikia na kuyajibu maombi yetu. Moja ya hayo hali ya kuhitaji msaada toka Kwake. Ameahidi, “Kwa maana nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu” (Isaya 44:3). Wale wote wenye njaa na kiu ya haki, wenye shauku ya kumjua Mungu, wanaweza kuwa na uhakika kuwa watashibishwa. Moyo lazima uwe wazi kwa ajili ya mvuto wa Roho, vinginevyo baraka za Mungu haziwezi kupokelewa.

Hitaji letu kubwa lenyewe ni hoja na husihi kwa nguvu zaidi kwa niaba yetu. Lakini Bwana anapaswa kutafutwa katika maombi aweze kutufanyia mambo haya. Kwani anasema, ‘’ombeni nanyi mtapewa.’’ Tena “Yeye asiyemwachilia Mwana Wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja Naye” (Mathayo 7:7; Warumi 8:32)?

Ikiwa tukiwaza maovu mioyoni mwetu, kama tuking’ang’ania dhambi yoyote inayojulikana, Bwana hatatusikia; lakini maombi ya roho iliyopondeka na yenye toba hukubaliwa kila wakati. Wakati makosa yote yanayojulikana yanaposahihishwa, twaweza kuamini kuwa Mungu atajibu maombi yetu. Wema wetu sisi wenyewe hauwezi kutustahilisha kupata fadhila za Mungu; ni sifa stahilifu ya Yesu ndiyo itakayotuokoa, damu Yake ndiyo itakayotutakasa; lakini, hata hivyo, tunayo kazi ya kufanya ili kuendana na masharti ya kupokelewa.

Jambo lingine la msingi linalohusiana na maombi ni imani. “Mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba Yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Waebrania 11:6. Yesu aliwaambia wanafunzi Wake, “Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu” (Marko 11:24). Je, twamchukua Bwana kama alivyosema katika Neno Lake?

Hakuna Jambo Gumu Linalomshinda Mungu

Peleka mahitaji yako, furaha yako, huzuni zako, masumbufu yako, na hofu zako mbele ya Mungu. Huwezi kumwelemea kwa kumtwisha mzigo mzito; huwezi kumchosha. Yeye awezaye kuhesabu idadi ya nywele za kichwa chako hayapuuzii mahitaji ya watoto Wake. “Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma” (Yakobo 5:11). Moyo Wake wa upendo huguswa kwa huzuni zetu na hata kwa maneno yetu yanayozitamka. Peleka Kwake kila kinachoifadhaisha akili. Hakuna lolote lililo kubwa Kwake kulibeba, kwani hushikilia malimwengu, huyatawala mashauri ya ulimwengu wote. Hakuna chochote kinachohusu amani yetu ambacho ni kidogo sana Kwake kiasi cha kutokiona. Hakuna sura katika uzoefu wetu yenye giza sana Kwake kiasi cha kutoisoma; hakuna mfadhaiko ulio mgumu sana Kwake kiasi cha kutoitatua. Hakuna dhoruba iwezayo kumpata hata mmojawapo mdogo kabisa miongoni mwa watoto Wake, hakuna hofu inayoisumbua roho, hakuna furaha, hakuna maombi ya dhati yatokayo midomoni, ambayo Baba yetu wa mbinguni hayatazami, au ambayo havutiwi nayo. “Huwaponya waliopondeka moyo, kuziganga jeraha zao.” Zaburi 147:3. Uhusiano kati ya Mungu na kila nafsi ni wa pekee na kamilifu kabisa kiasi kwamba kama kusingekuwa na mtu mwingine duniani kushiriki kupata uangalizi Wake, kiasi kwamba kama kusingekuwa na mtu mwingine ambayo kwa ajili yake alimtoa Mwanawe Mpendwa.

*Imenukuliwa toka kitabu cha Steps to Christ au Njia Salama (Amani katika Dhoruba, Hatua za Ushindi.