Kuvunja Mazoea Mabaya

 

Miaka kadhaa iliyopita nilimtembelea rafiki yangu ambaye niliwahi kutumia madawa ya kulevya pamoja naye. Yeye, kama mimi na mke wangu Susan, tulikuwa tumetumia madawa ya kulevya katika maisha yetu yote ya utu uzima, tangu miaka ya 1972. Mimi na Susan tuliacha kutumia madawa hayo mwaka 1996; hata hivyo, rafiki yangu Randy hakuwa na bahati hiyo.

Nilipomtazama alionekana kukaribia mauti. Baada ya kukumbatiana kwa muda mrefu nilimtazama machoni. Nilimwona akianza kutokwa machozi. Aliniambia jinsi nilivyoonekana nadhifu, na jinsi alivyokuwa na furaha kwamba nilikuwa nimeacha kutumia madawa ya kulevya na pombe. Nilimtazama kwa huzuni na kusema, “Randy, hupaswi kuishi hivi.” Alinitazama kwa mshangao na kuniuliza, “Sipaswi?” Hakuna mtu yeyote aliyewahi kumwambia hivyo hapo kabla; Randy hakujua njia nyingine zaidi. Lakini hapa kuna habari njema—hakuna mtu yeyote anayepaswa kuishi kwa kutawaliwa na mazoea mabaya (uraibu), ukiwemo wewe.

Kwa baadhi ya watu maisha yao yote ni ya kutafuta dawa za kutuliza maumivu. Maumivu huja kwa namna mbalimbali (kihisia na kimwili) na mara nyingi kwa wanadamu, ndivyo ilivyo pia utulizaji wa maumivu (uraibu kwa njia ya madawa ya kulevya, pombe na sigara) utokeavyo. Amini usiamini, mazoea mabaya mara nyingi ni njia ya kujaribu kukabiliana na maumivu. Njia za kujaribu kukabiliana, ambazo watu wanatumia ili kuendelea na maisha ni za aina mbili: matumizi mabaya ya madawa na tabia mbaya kwa watu, ambazo hujulikana vizuri kama uraibu wa madawa na uraibu wa kitabia.

Madawa ambayo hutumiwa vibaya ni kama bangi, dawa za mitaani, pombe, tumbaku na kafeini, pamoja na dawa za hospitalini za kuzuia maumivu. Uraibu wa tabia ni mpana sana na mgumu kuuelezea. Hujidhihirisha katika njia nyingi kuanzia kamari, hadi hasira, uraibu wa ngono, wivu, umbea, uraibu wa vyombo vya habari, uraibu wa vyakula, kufanya kazi kupita kiasi, au tabia nyingine yoyote wanayoweza kuwa nayo watu ambayo huwaondoa mbali na uhalisia.

MATATIZO TANGU MWANZO

Mara nyingi, chanzo cha uraibu kinaweza kupatikana wakati wa utotoni. Ingawa hukuwa unafahamu, kipindi cha awali cha maisha yako, ubongo wako ulikuwa unajenga uwezo wake na kemikali ambazo zilikuwa zinakwenda kukuwezesha kukabiliana na maisha pamoja na changamoto zake. Kama uwezo huu haukujengeka kikamilifu kwa sababu yeyote ile (vitendo vya ukatili, matusi, kupuuzwa, kutumiwa vibaya kijinsia na mengineyo), ungejikuta ukitafuta njia zingine za kukabiliana na maisha.

Unaweza kujikuta uko katika hali hii hivi sasa, bila kujua, ukijaribu kushughulikia maumivu na hisia za mfadhaiko za wakati uliopita. Unatafuta kitulizi cha maumivu kupitia tabia au vitu ambavyo unajua sio vizuri kwako, na wakati huohuo hicho ndio kitu pekee kinachoweza kukupatia nafuu. Na unasema moyoni mwako, hivi mtu anaweza kuninyang’anyaje kitu hiki? Hii ndio njia pekee ya kukabiliana na maisha. Nyakati zingine huwezi hata kutambua maumivu na matatizo unayoyakimbia, na hiki ndicho kitu hasa kinachofanya aina hii ya mazoea mabaya kuwa vigumu kuacha.

Aina nyingine ya mazoea mabaya hutokana na kukuza tu tamaa zako za asili za kibinadamu. Mazoea haya yanaweza kuunda minyororo inayokufunga kwa nguvu sana kama aina nyingine ya uraibu. Aina zote za mazoea mabaya mara nyingi huonekana kuwa hali ya kukatisha tamaa, na niamini rafiki, nimewahi kuwa kwenye hali hiyo. Uraibu wako huu ni mazoea yanayokutawala; huwezi kuyatawala. Mazoea hayo hukwambia wakati na mahali pa kuyatekeleza. Kila wakati unapofanya uamuzi kwa ajili ya kuendelea au kuachana na mazoea ya tabia mbaya ya uraibu, njia za fahamu huundwa kwenye ubongo zinazoimarisha zaidi mazoea hayo mabaya.

KUSHINDA MAZOEA MABAYA

Kwa hiyo, tunabadilishaje njia za kukabiliana? Au tunajinasuaje kutoka kwenye mazoea ya tamaa ambayo yamepenya ndani kabisa kwenye njia zetu za fahamu na kuachana na mazoea ya tamaa za mwili? Tunawezaje, kwenye akili zetu, kujitengenezea maisha yetu mapya ya baadaye? Kulijibu swali hilo kikamilifu kwa kila mtu kuko nje ya uwezo wa kijuzuu hiki kidogo. Kila hali ni ya pekee, na sehemu kubwa ya mchakato wa kupata nafuu unahitaji umakini na ushauri binafsi, baadhi zinaweza kupatikana mwishoni wa kijuzuu hiki. Lakini hatua ya kwanza, ambayo hufanana katika njia zote fanisi kuelekea kwenye hali njema, ni kutambua kuwa hupaswi kuishi na mazoea mabaya na kutambua chanzo cha ufumbuzi wa tatizo.

Tunaye Baba mbinguni ambaye hataki tuishi maisha yetu tukiwa tumefungwa kwenye mazoea yetu mabaya. Anahitaji tuishi maisha huru, yenye furaha, na afya njema. Anahitaji tujifunze jinsi ya kuyaachilia matatizo yetu ya zamani katika siku hizo za nyuma. Anaweza kuwa njia yetu nzuri na mpya ya kukabiliana na matatizo. Anataka vitu hivi vizuri viwe vyetu kiasi cha kumtoa Mwanawe, na kupitia Zawadi hiyo alitupatia uwezo wote unaohitajika ili kuepuka minyororo inayotufunga. Sikiliza ahadi Yake: “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili” (1 Wakorintho 10:13). Uhuru unawezekana na hata umeahidiwa! Mungu anaweza kuvunja mzunguko wa mazoea mabaya katika maisha yako! Anaweza “kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa Yeye” (Waebrania 7:25).

Je, kushindwa mara kwa mara kumeondoa tumaini ndani yako? Kujikita katika ukosefu wako wa uwezo na juu ya kushindwa kunakatisha tamaa, lakini kumtazama Mungu na kuamini nguvu Zake huyarudisha matatizo kwenye mtazamo sahihi. Angalia uhalisia kwa muda fulani. Mtu ambaye una mwelekeo wa kumwamini zaidi ni wewe mwenyewe. Tatizo ni kuwa tumethibitisha tena na tena kwamba hatufanyi kazi nzuri sana ya kuyasimamia maisha yetu. Ili kulieleza kwa usahihi, tumemwamini mtu asiye sahihi. Katika Mithali 3:5, Biblia inasema “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.” Mungu analisema hali kwa sababu fulani. Anajua kuwa ufahamu wetu umepotoka, anajua kuwa tumeharibika kihisia, anajua kuwa tunafanya kadri ya uwezo wetu, lakini pia anajua kuwa tunahitaji kumwamini na kuuamini uweza Wake—vinginevyo matumaini yetu na hamasa yetu hutoweka. Mungu ana mpango mpya alioandaliwa kwa ajili yetu, njia ya hatua kwa hatua ili kuondoa tabia mbaya na kutuwezesha kutenda tabia njema, njia ya kubadili neva hizo za fahamu kwenye ubongo ili ziweze kuwa bora daima, ili ziweze kuwa na manufaa kwetu na wala sio kutudhuru.

Wakati fulani Yesu alimwuliza kipofu, “Wataka nikufanyie nini?” (Marko 10:51). Yule kipofu akamwambia, “Nataka nipate kuona.” Ili kufupisha, Yesu alikuwa anamwuliza mtu huyo endapo alitaka kuponywa. Na leo, swali kama hilo linaulizwa kwako, rafiki. Hupaswi kuishi namna hii. Je, unahitaji kuponywa? Je, unahitaji kusoma maelezo ya kuponywa yanayopatikana mwishoni mwa kijizuu hiki? Je, unahitaji kusimama tena na kusonga mbele kuelekea kwenye uhuru na amani? Wewe peke yako ndiye uwezaye kulijibu swali hilo.

MASOMO YALETAYO USHINDI

Aina fulani maalum za mazoea mabaya huweza kudhibitiwa kirahisi zaidi kwa mpango wa muda mrefu ulioandaliwa vizuri. Hapa chini kuna baadhi ya tovuti maalum zinazosaidia kushinda tabia mbalimbali zenye mazoea mabaya. Kumbuka kuwa Mungu anaweza kuwaokoa kabisa wote wamwendeao Yeye kupitia Kristo! Ushindi unawezekana kupitia imani katika Mungu, mabadiliko ya kivitendo, nia thabiti, na juhudi!

Ulevi wa Pombe: http://www.aa.org

Madawa ya Kulevya: http://www.na.org, http://www.justasiamministries.com

Uraibu wa Kingono: http://www.purelifeministries.org, http://www.saa-recovery.org

Uraibu wa Kamari: http://www.gamblersanonymous.org