Kile Ambacho Ulimwengu Unakihitaji Sasa

Kila mtu katika dunia hii anahitaji upendo wa kweli. Ulimwengu una tafsiri nyingi za upendo, lakini tunahitaji upendo wa kweli.

Biblia Takatifu inatuambia kuwa “Mungu ni upendo” (1 Yohana 4:8). Si hivyo tu, bali pia hutuambia kuwa Muumba wa Dunia anao ujumbe maalum wa upendo ulioandaliwa kwa namna ya pekee kwa ajili ya “siku hizi za mwisho” (2 Timotheo 3:1). Ujumbe wake wa siku za mwisho hujumuisha upendo na sheria (tazama Ufunuo 14:12-14) kutokana na sababu rahisi kuwa upendo wa kweli ni suala la kimaadili. Kwa maneno mengine, upendo unahusisha jambo la kina zaidi ya hisia zisizokuwa na tendo.

Kila taifa, serikali, utawala, jiji, na mji una sheria. Bila sheria, vurugu hutawala. Lakini kuna sheria moja ambayo ni kuu zaidi ya zingine zote: Amri Kumi. Kinachofanya Amri Kumi kuwa tofauti na sheria zingine ni kwamba zilipoandikwa mara ya kwanza si kwa kalamu, penseli, kiibodi, au kompyuta, bali “kwa chanda cha Mungu” mwenyewe (Kutoka 31:18). Soma Kutoka 20:1–17 ili kupata kisa kamili. Kwa ufupi, zifuatazo ni Amri Kumi kwa lugha rahisi:

1. Mtangulize Mungu.

2. Usiabudu sanamu.

3. Liheshimu Jina la Mungu.

4. Ishike siku ya Sabato (Jumamosi) na kuitakasa.

5. Mheshimu baba yako na mama yako.

6. Usiue.

7. Usizini.

8. Usiibe.

9. Usiseme uongo

10. Usitamani.

Hebu jaribu kufikiria jinsi ambavyo jamii ingekuwa endapo kila mtu kwa hakika angezifuata amri hizi kwa ukamilifu. Wezi wasingekuwepo. Wala wauaji au hata watu wachoyo. Magereza, makufuli milangoni, au hata polisi wasingehitajika. Magaidi au mabomu ya kufisha yasingekuwepo. Badala yake, wanadamu wote wangetendeana kwa staha, wema, na heshima. Katika mazingira kama hayo, familia zingestawi, watoto wangekua wakiwa salama, na furaha ingeuburudisha kila moyo.

Je, kweli jambo hili linaweza kutokea? Najua inaweza kuonekana vigumu kuamini jambo hili kwa kuwa tunaishi kwenye ulimwengu uliojaa dhambi, lakini Biblia hutabiri kuwa siku moja jambo hili litatokea. “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya” (Ufunuo 21:5), anaahidi Mungu Mwenyezi. Si hilo tu, bali pia unaweza kuishi milele katika Paradiso hiyo, ikiwa utaelewa tabia ya Mungu ya upendo wa kweli na kufanya uchaguzi sahihi. Ngoja nitoe maelezo.

Siri imefichwa ndani ya unabii wa zamani kuhusu Yesu Kristo. “Na jina Lake atakaloitwa ni hili, BWANA NI HAKI YETU” (Yeremia 23:6). Neno, “haki,” au “kutenda mema,” kwa maneno rahisi humaanisha kuzifuata Amri Kumi, “sheria ya haki” (angalia Warumi 9:31) bila kasoro yoyote. Ni dhahiri, hakuna yeyote miongoni mwetu ambaye amewahi kufikia kiwango hicho au kufanya hilo. Badala yake, “wote wamefanya dhambi” (Warumi 3:23). Lakini habari njema ni kwamba takriban miaka elfu mbili iliyopita—katika tendo lililotokana na upendo wa hali ya juu kabisa—Yesu alitunza Amri Kumi (angalia Yohana 15:10) kwa ajili yetu, kwa niaba yetu. Matokeo yake, sasa Yeye ni “BWANA ALIYE HAKI YETU.”

Lakini hapa kuna habari mbaya ambazo hatuwezi kuziepuka. “Mshahara wa dhambi ni mauti” (Warumi 6:23). Kwa maneno mengine, adhabu ya kuvunja Amri Kumi ni uangamivu wa milele. Haki inahitaji jambo hilo litendeke. Hakuna njia ya kulikwepa. Kwa upande mwingine, hapa kuna habari nyingine njema: Mwishoni mwa maisha Yake duniani, “Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu” (1 Wakorintho 15:3) pale msalabani mahali petu pia, ikiwa na maana kuwa anaweza sasa kutusamehe, kuondoa hatia zetu, na kutusafisha!

Je, unafurahia kupokea zawadi? Watoto wangu, wenye umri wa miaka 5 na 8, kwa kweli hulifurahia hilo. Ni mtoto yupi asiyependa? Mungu Mwenyezi ametoa bure “kipawa cha haki” katika Kristo Yesu (angalia Warumi 5:17) kwa ajili yako kinachoweza kukupatia “uzima wa milele” (angalia Warumi 6:23). Kama uko tayari kugeuka na kuacha dhambi na kumwamini Yesu kama Mwokozi wako, ataweka utii kamilifu wa Yesu kwa Amri Kumi mahali pa dhambi zako katika vitabu Vyake vya kumbukumbu mbinguni (angalia Ufunuo 20:12). “Si Mkosaji!” “Hana Kosa!” “Amesamehewa!” yatakuwa ndiyo maneno yatakayotamkwa kwako na Mfalme wa Ulimwengu, bila kujali makosa au dhambi gani umetenda. Hili huturejesha kwenye utafutaji wa pamoja wa upendo halisi.

Hapa kuna kisa kinachotoa maelezo: Siku moja kijana fulani asiyejali alikuwa na majibizano makali na baba yake. Maneno yake ya mwisho yalikuwa, “Ninaondoka. Hutaniona tena kamwe!” wakati akiondoka pale nyumbani. Yule kijana alidhani angeliweza kuishi kwa uwezo wake mwenyewe, lakini baada ya miaka mitatu ya taabu, kwa huzuni, mawazo yake yakageukia nyumbani kwao. Je, baba yangu atanikubali tena? Alijiuliza kwa hofu. Siku mbili baadaye, hatimaye yule kijana akapata ujasiri wa kumpigia simu mama yake. “Mama, tafadhali zungumza na baba. Mwambie nitakuwa nikipita chini ya kilima chetu kwa treni siku ya Jumatatu ijayo jioni. Mwambie aning’inize kitu fulani cheupe barazani ikiwa anapenda nirudi. Kama nitaona kitu chochote cheupe, nitakuja nyumbani.” Kisha akakata simu.

Jumatatu hiyo asubuhi, kijana yule mwenye hofu alipanda treni, na ikatokea kwamba alikaa karibu na mchungaji. “Kwa nini una wasiwasi hivi?” mchungaji alimwuliza. Kisha yule kijana akamweleza kisa chote. “Bwana,” alisema, “tutakapokuwa tukikata kona iliyoko mbele yetu, unaweza kutazama kupitia dirishani nyumba iliyo juu ya mlima? Hiyo ni nyumba yangu. Ikiwa utaona kitu chochote cheupe, niambie. Ninaogopa kutazama!”

Wakati treni ikimalizia kukata kona ya mwisho na mchungaji alipoangalia kupitia kioo cha dirisha, mwonekano huo ulimfanya kusahau hadhi yake ya kichungaji. Huku akiruka, mchungaji huyu alipaza sauti, “Angalia kijana, angalia!” Alipofumbua macho yake, yule kijana akaiona nyumba ndogo mlimani ikiwa imefunikwa kabisa na kila kitambaa cheupe ambacho wazazi wake walikuwa nacho: blanketi nyeupe, taulo nyeupe, shuka jeupe, na kitambaa cheupe cha mezani, kitambaa cha mikono cheupe na leso nyeupe. Jinsi gani walimpenda na walitaka arudi nyumbani. Kitu cha mwisho alichoona yule mchungaji kuhusiana na yule kijana ni miguu yake ikikimbia haraka kukwea kile kilima, akivuka ile kona, akivipita vile vitambaa vyeupe, hadi katika mikono ya wazazi wapweke iliokuwa inamsubiri.

Ndugu msomaji, Yesu anakupenda na anahitaji urudi nyumbani vilevile. Kwa hiyo tubu dhambi zako, kisha mwamini Yeye kama Mwokozi wako. Kama ukimwamini, atakuvika “vazi la haki” Yake mwenyewe (angalia Isaya 61:10), “mavazi Yake meupe” (angalia Ufunuo 3:18) ya msamaha kamili, bila kujali jinsi maisha yako ya zamani yalivyokuwa maovu. Anaahidi kuwa atatenda (angalia 1 Yohana 1:9). Unaweza kumwamini kwa hili.

“Ulikuja na kubisha hodi kwenye mlango wa moyo wangu. Wewe ni kila kitu ambacho nimekuwa nikikitafuta.” Maneno haya kwa kweli yanamhusu Yesu Kristo pekee, Mwokozi wako.

Yeye ndiye zawadi yako ya upendo kutoka kwa Mungu.

Kupitia zawadi ya haki Yake—ambayo ndiyo pekee iwezayo kufunika dhambi za kuvunja Amri Kumi—unaweza kuwa na “uzima wa milele” katika siku ya Mungu yenye utukufu mahali ambapo upendo pekee hutawala (angalia Ufunuo 21:4, 5).

Swali kubwa ni: Je, utatubu, na kuikubali zawadi hiyo, au la?