Yachunguzeni Maandiko Somo la 09 – Waliokufa Wako Wapi?

Nilihudhuria ibada moja ya mazishi ambayo ilianza kwa muziki wa taratibu. Baada ya kusoma Maandiko na kuomba, Mchungaji alianza kuhubiri.

Aliwahakikishia waombolezaji kuwa marehemu alikuwa hajafa kabisa. Alikuwa mzima na alikuwa mbele za Mungu. akaendelea kutushawishi kuwa mtu ambaye alikuwa ametangazwa na madaktari kuwa amekufa, alikuwa akitazama toka mbinguni na kuona kila kitu kilichokuwa kinaendelea kwenye ibada hiyo ya mazishi. Marehemu alidhaniwa kuwa yuko kwenye hali bora zaidi ya maisha.

Nilishtushwa sana na baadhi ya madai yaliyokuwa yanatolewa na mchungaji huyo. Niligundua pia kuwa madai yake hayakuungwa mkono na mafungu yo yote ya Biblia. Hubiri lake lilikuwa mfano mzuri wa nadharia na utata ulio katika ulimwengu wa kidini kuhusu suala la kifo.

Je, mtu akifa, anakuwa na hali gani? Tunajua kitu juu ya uzima, kwamba ni nini na una maana gani. Lakini ni jambo gani linalotokea tunapokufa? Tunakwenda wapi? Mbinguni? Jehanum? Toharani? (Toharani ni mahali ambapo baadhi ya watu hudai marehemu hupitia kupata mateso ili aruhusiwe kuingia ahera) au Ahera? Ndugu zetu waliokufa wako wapi? Je, tunaweza kuwaona? “Mtu akifa, je! atakuwa hai tena?” (Ayu. 14:14).

Kwa nini tusiigeukie Biblia? Fundisho la Biblia juu ya kifo ni thabiti na halina utata. Unaweza kushangaa. Lakini majibu yake yanaeleweka, yanaridhisha, na zaidi ya yote, yanafariji.

1. Kwanza kabisa tuliumbwa namna gani?

“BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwa. 2:7.

Tuliumbwa kwa mavumbi.

2. Mtu anapokufa, huwa kunatokea nini?

“Nayo mavumbi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa.” Mhu. 12:7.

Mwili huyarudia mavumbi na roho humrudia Mungu aliyeitoa. Roho ya mtu aliyekufa, awe mwenye haki au mwovu – humrudia Mungu wakati wa kufa.

3. Roho inayomrudia Mungu ni kitu gani?

“Mwili pasipo roho umekufa.” Yak. 2:26. “Roho ya Mungu i katika pua yangu.” Ayu. 27:3.

Roho inayomrudia Mungu wakati wa kufa ni ile pumzi ya uhai. Hakuna mahali katika Biblia ambapo roho inaelezwa kuwa ina uhai, hekima au hisia baada ya mtu kufa. Ni “pumzi ya uhai”, si zaidi.

4. Nafsi ni nini?

“BWANA Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwa. 2:7.

Nafsi ni kiumbe chenye uhai. Nafsi mara zote ni muungano wa vitu viwili: Mwili na pumzi. Nafsi haiwezi kuwepo bila mwili na pumzi kuunganishwa. Neno la Mungu linafundisha kuwa sisi ni nafsi.

5. Je, Nafsi inaweza kufa?

“Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa.” Eze. 18:20. “Vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa.” Ufu. 16:3.

Kulingana na Neno la Mungu, nafsi inaweza kufa! Sisi ni nafsi na nafsi zinaweza kufa. Mwanadamu hufa. Mungu pekee hapatikani na mauti (1 Tim. 6:15,16). Dhana ya nafsi isiyokufa inapingana na Biblia inayofundisha kuwa nafsi hazina budi kufa.

6. Je, watu wema huenda mbinguni baada ya kufa?

Mungu alisema, “Hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.” Mwa. 3:19.

“Watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake… Nao watatoka.” Yn 5:28,29. “Daudi… alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo.” “Maana Daudi hakupanda mbinguni.” Mdo. 2:29,34. “Nikitazamia kuzimu (kaburi) kuwa nyumba yangu.” Ayu. 17:13.

Watu hawaendi mbinguni wala Jehanum baada ya kufa. Wanaenda kaburini kusubiri ufufuo.

7. Je, mtu aliyekufa anaweza kujua au kuelewa kiasi gani?

“Walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote linalofanyika chini ya jua.” “Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu (kaburini) uendako wewe.” Mhu. 9:5,6,10. “Sio wafu wamsifuo BWANA.” Zab. 115:17.

Mungu anasema wafu hawajui kitu cho chote.

8. Lakini, je! wafu hawawezi kuwasiliana na walio hai, na je! hawajui mambo ambayo walio hai wanayafanya?

“Ni vivyo mwanadamu hulala chini, asiinuke; hata wakati wa mbingu kutokuwako tena, hawataamka, wala kuamshwa usingizini.” “Wanawe hufkilia heshima, wala yeye hajui; kisha wao huaibishwa, lakini yeye hana habari zao.” Ayu. 14:12,21. “Wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua.” Mhu. 9:6.

Wafu hawawezi kuwasiliana na walio hai. Wamekufa. Mawazo yao yamepotea (Zab. 146:4).

9. Yesu aliita “usingizi” hali ya kutokujitambua kwa waliokufa katika Yn. 11:11-14. Je, watalala kwa muda gani?

“Ni vivyo mwanadamu hulala chini, asiinuke; hata wakati wa mbingu kutokuwako tena.” Ayu. 14:12. “Siku ya Bwana itakuja… katika siku hiyo mbingu zitatoweka.” 2 Pet. 3:10.

Wafu watalala hadi siku ile kuu ya Bwana, mwisho wa dunia. Katika mauti wanadamu hawajitambui kabisa, hawawezi kufanya jambo lo lote wala kuwa na maarifa ya aina yo yote ile.

10. Litawatokea jambo gani wenye haki waliokufa, wakati wa kuja kwa Yesu mara ya pili?

“Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.” Ufu. 22:12. “Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko,… nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza… na hivyo tutakuwa na Bwana milele.” 1 Thes. 4:16,17. “Sote tutabadilika, kwa dakika moja, kufumba na kufumbua,… na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu… Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa. Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika…” 1 Kor. 15:51-53.

Kusingekuwa na haja ya ufufuo kama waliokufa wanakwenda mbinguni baada ya kufa.

11. Uongo wa kwanza kabisa wa Ibilisi ni upi?

“Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa.” Mwa. 3:4. “Yule joka… yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote.” Ufu. 12:9.

Shetani alimwambia Hawa kwamba dhambi isingeleta mauti. Alisema, “Hakika hamtakufa.”

“Ni vivyo mwanadamu hulala chini, asiinuke; hata wakati wa mbingu kutokuwako tena.  Ayu. 14:12

 

12. Ni kwa nini Shetani alisema uongo kuhusu kifo? Je, inawezekana kuna sababu ya muhimu kuliko wengi wanavyofkiri?

Ni moja kati ya mafundisho ya msingi ya ufalme wa Ibilisi. Amekuwa akifanya miujiza katika vizazi vyote kwa kutumia watu wanaodai kuwa wanapata uwezo wao toka kwa roho za waliokufa (k.m. Wachawi wa Misri – Kut. 7:11; Mwanamke wa Endori – 1 Sam.28:3-25; Wachawi – Dan.2:2; Kijakazi mwenye pepo wa uaguzi – Mdo. 16:16-18).

Onyo Muhimu
Katika siku za mwisho Shetani atatumia tena uchawi – kama alivyofanya wakati wa Danieli – kudanganya ulimwengu (Ufu. 18:23). Uchawi ni wakala wa miujiza unaodai kuwa unapata nguvu na hekima toka kwa roho za waliokufa.

Watakuja Kama Wanafunzi wa Yesu
Shetani na malaika zake watawadanganya mabilioni ya watu kwa kuja kama wapendwa waliomcha Mungu waliokufa, wachungaji wacha Mungu ambao sasa wamekufa, manabii wa Biblia, au hata mitume au wanafunzi wa Kristo (2 Kor. 11:13-15). Wanaweza pia kuja kama watu maarufu waliokufa kama wafalme na Maraisi. Wale wanaosadiki kwamba wafu wako hai, katika umbile lo lote lile, kwa hakika watadanganyika kabisa.

13. Je, mashetani hufanya kweli miujiza?

“Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara” Ufu. 16:14. “Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.” Mt. 24:24.

Ndiyo, mashetani hufanya miujiza ya kuaminika ajabu! (Ufu.13:13,14). Shetani na malaika zake hujigeuza kuwa malaika wa nuru (2 Kor. 11:14), na, mbaya zaidi, hujigeuza kuwa Kristo mwenyewe (Mt. 24:23,24).

14. Kwa nini watu wa Mungu hawatadanganyika?

“Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.” Ufu. 3:10. “Walilipokea lile Neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza Maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo.” Mdo. 17:11. “Ikiwa hawasemi sawasawa na Neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi (hawana nuru ndani yao, KJV).” Isa. 8:20.

Kutokana na kusoma kwa makini Neno la Mungu, watu wa Mungu watajua kuwa wafu wamekufa, hawako hai. Hakuna roho za waliokufa. Watu wa Mungu hawatakubaliana na fundisho lo lote linaloonyesha kuwa wafu wako hai na hawatakubaliana na miujiza inayodaiwa kufanyika kwa uwezo wa roho za waliokufa.

15. Wakati wa Musa, Mungu aliamuru watu wanaofundisha kuwa wafu wako hai wafanywe nini?

“Tena mtu mume au mtu mke aliye na pepo, au aliye mchawi, hakika atauawa; watawapiga kwa mawe.” Law. 20:27.

Mungu alisisitiza kuwa wachawi na wengine waliokuwa na pepo (waliodai kuwa wanaweza kuwasiliana na waliokufa) ni lazima wauawe.

16. Je, wenye haki watakaofufuliwa, watakufa tena?

“Wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu,… hawawezi kufa tena.” Lk. 20:35,36. “Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti hitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.” Ufu. 21:4. “Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu.” Ufu. 20:6.

Kifo, huzuni, kilio na majanga havitakuwepo katika ufalme mpya wa Mungu.

Tumejifunza katika swali la 11 na 12 kuwa Shetani ndiye aliyebuni fundisho kuwa wafu wako hai. Kuwasiliana na mizimu, ibada ya mizimu, na nafsi isiyokufa ni uzushi wa Shetani, akiwa na lengo moja. Kuwafanya watu waamini kuwa wafu wako hai.

Watu wanapoamini kuwa wafu wako hai, hizo huwa ndizo “roho za mashetani zifanyazo ishara” (Ufu. 16:14) na kujifanya roho za waliokufa, nazo zitaweza kuwadanganya na kuwapotosha kabisa wakati wote.

Je, unamshukuru Mungu kwa ajili ya Biblia inayotuambia ukweli kuhusu somo hili muhimu?

Je, ungependa Mungu akusaidie ili uweze kuzitambua hila za Mwovu kwa kuyachunguza Maandiko kila siku?