Yachunguzeni Maandiko Somo la 04 – Mahakama Ya Mungu

Nimewahi kusikiliza kesi ya mauaji wakati fulani. Katika kesi ambayo hukumu yake ni kifo, mshitakiwa pamoja na wakili wake hupima kila kipengere cha ushahidi unaotolewa kwani hatima yake inaweza kutegemea kauli ya shahidi mmoja tu.

Mshitakiwa alikuwa akisikiliza kwa makini ushahidi uliokuwa unatolewa na hisia mbalimbali zilikuwa zikipita ndani yake. Hisia za kutisha na zingine zinazohitilafana za matumaini na za kukata tamaa kila aliposikia ushahidi ukitolewa ama dhidi yake, ama dhidi ya wa kumtetea. Hali ilikuwa ngumu zaidi baada ya pande zote kusikilizwa, na Jopo la Majaji kwenda faragha ili kufanya uamuzi. Waliporudi hukumu ilisomwa. Ilikuwa furaha iliyoje mshitakiwa aliposikia, “Hana hatia.” Kama hukumu ingesema, “Ana hatia” ingekuwa huzuni na majuto makuu kwa mshitakiwa.

Rafki yangu, je, unajua kwamba kuna mahakama inayoendelea sasa ambayo inatuhusu mimi na wewe? Kila mtu, mdogo kwa mkubwa, aliyewahi kuishi duniani, amepangiwa kusimama mbele ya Mahakama hiyo. Mbele ya Kiti cha Hukumu cha Kristo. Hakuna anayeweza kukwepa. Jambo la msingi ni kujiuliza, “Je, tuko tayari kusimama mbele ya Kiti cha Hukumu na kusikia hukumu ikitolewa?

Tukitambua umuhimu wa hukumu inayotukabili, ni vizuri tukaachana na mahangaiko ya dunia hii na kuangalia jinsi Biblia inavyosema juu ya tukio hili muhimu.

1. Je, tunajuaje kuwa kutakuwa na hukumu?

“Kwa maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika wafu.” Mdo. 17:31.

2. Ni akina nani watakaosimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo?

“Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha kukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.” 2 Kor. 5:10.

Kila mtu! Sisi sote! Hakuna atakayekwepa. Watu wa kila kabila, taifa na watu wa madhehebu yote! Uamuzi wa mahakama hii ni wa mwisho. Hakuna rufaa! Kila mmoja wetu lazima akutane na Mhukumu Mkuu uso kwa uso! Kila mmoja wetu ana nafsi ya kuiokoa au kuipoteza!

3. Katika hukumu hii, hakimu ni nani?

“Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye Mzee wa Siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu saf; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunguliwa.” Dan. 7:9,10.

Mzee wa Siku. Mungu mwenyewe atakuwa hakimu!

4. Zaidi ya Mungu, nani mwingine aliye ndani ya Mahakama hiyo?

“Maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunguliwa.” Dan. 7:10.

Malaika, maelfu elfu na elfu kumi mara elfu kumi watakuwepo katika mahakama. Hawa ndio mashahidi waliokuwa wakishuhudia mambo yote ya wanadamu.

5. Wakati Mahakama imeshakaa nani analetwa mbele za Mungu?

“Tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo Mzee wa Siku, wakamleta karibu naye.” Dan. 7:13.

Aliye mfano wa mwanadamu. Yesu mwenyewe anasimama katika Mahakama mbele za Mungu.

6. Yesu anasimama kama nani katika Mahakama?

“Tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki.” 1 Yoh. 2:1.

Mwombezi, Mtetezi. Yesu atasimama mahakamani kama wakili wa wale wote waliompokea.

7. Je, kama kuna Wakili upande wa utetezi, upande wa mashtaka atakuwapo nani?

“Ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.” Ufu. 12:10.

Mshitaki atakuwa Shetani akidai kuwa wanadamu wote wametenda dhambi, na kwa hiyo wanapaswa kwenda motoni pamoja naye.

8. Mshitakiwa ni nani?

“Imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo.” 2 Kor. 5:10.

Wanadamu! Mimi na wewe! Lakini hatutalazimika kusimama wenyewe katika hukumu. Kristo yuko tayari kusimama mbele ya kiti cha enzi kama wakili wa wote waliotubu dhambi zao, na ambao kwa imani wameipokea damu yake kama kafara ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zao.

Yesu mwenyewe, Mwumbaji na Mkombozi wetu ni wakili wa utetezi katika Mahakama ya Mungu.

9. Tunapaswa kufanya nini ili Yesu ayakiri majina yetu mbele za Baba yake?

“Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.” Mt. 10:32.

Ni lazima kwanza tumkiri yeye mbele za watu kuwa ni Mwokozi na Bwana wetu.

10. Kitatumika kigezo gani katika kuwahukumu wanadamu?

“Mtu awaye yote atakayeishika Sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja Sheria. Semeni ninyi, na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa Sheria ya Uhuru.” Yak. 2:10-12.

Katika mahakama za kidunia, watu huhukumiwa kwa sheria za nchi au serikali. Katika mahakama ya Mungu watu watahukumiwa kwa Amri Kumi za Mungu. Ni lazima viwepo vigezo vya kupima matendo ya watu kabla mtu hajaonekana na hatia au la. “Pasipokuwapo Sheria, hapana kosa.” Rum. 4:15. Kigezo kitakachotumika ni Sheria ya Mungu.

11. Ni mambo gani yatakayoangaliwa katika hukumu?

“Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.” Mhu. 12:14. “Atayamulikisha yaliyositirika ya giza, na kuyadhihirisha mashauri ya mioyo.” 1 Kor. 4:5. “Wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.” Ufu. 20:12.

Matendo, maneno, mawazo na hata makusudi yaliyosababisha kila jambo yataangaliwa katika hukumu.

12. Je, ni kitu gani kitatumika kama ushahidi?

“Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake… Vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima… wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao… Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake…. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.” Ufu. 20:11-15.

Mambo yaliyoandikwa kwenye vitabu. Hakutakuwa na kufcha wala kujitetea kwa uongo. Kila kitu kitakuwa kimeandikwa! Mungu hahitaji vitabu ili ajue mambo yetu, lakini yameandikwa kwa ajili yetu, ili tujue alivyojishughulisha na kila mwanadamu kwa uaminifu. Hatutakuwa na haja ya kuwa na mashaka juu ya wema na upendo wa Mungu. Ushahidi wote utakuwepo!

“Imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo.” 2 Kor. 5:10. 

13. Majina ya watu waliompokea Yesu yanaandikwa katika kitabu gani?

“Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana walishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima.” Flp. 4:3. “Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.” Lk. 10:20.

14. Je, jina la mtu aliyempokea Yesu na baadaye kurejea kwenye maisha ya dhambi linaweza kufutwa kwenye Kitabu cha Uzima?

“Musa akarejea kwa BWANA akasema, Aa! watu hawa wametenda dhambi kuu wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao – na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichoandika. BWANA akamwambia Musa, Mtu ye yote aliyenitenda dhambi ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu.” Kut. 32:31-33. “Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolitenda, atakufa.” “Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, akafa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa.” Eze. 18:24,26.

Ndiyo. Hatua ya kumwacha Yesu na kurudia maisha ya dhambi husababisha jina la mtu huyo kufutwa toka katika Kitabu cha Uzima.

15. Je, washindi dhidi ya dhambi wameahidiwa nini?

“Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, wala sitalifuta kamwe jina lake katika Kitabu cha Uzima, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele ya malaika zake.” Ufu. 3:5.

16. Je, hukumu hii itaanzia kwa nani?

“Kwa maana wakati umefka wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu; na ikianza kwetu sisi, mwisho wao wasioitii Injili ya Mungu utakuwaje?” 1 Pet. 4:17.

Katika nyumba ya Mungu, ambayo ni kanisa. (Nyumba ya Mungu ni Kanisa lake, yaani, watu wake – 1 Tim. 3:15).

17. Wale walioomba na kupokea msamaha wake wanahakikishiwa jambo gani?

“Nitawasamehe maovu yao, na dhambi zao sitazikumbuka tena.” Ebr. 8:12.

Dhambi zao hazitakumbukwa katika hukumu. Watahesabiwa wema na haki ya Kristo.

18. Hukumu hii itaanza lini?

“Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.” Ufu. 14:7.

Saa ya hukumu yake imekuja. Hukumu hii ni lazima ifanyike kabla Yesu hajaja kwani akija atakuwa tayari ana ujira wa kumlipa kila mtu. Tunaishi katika siku za “Saa ya Hukumu” ya Mungu. Majina ya watu mbalimbali yanapitiwa.

Je, umeshazungumza na wakili wa kukutetea?

Hebu angalia wakili mwenyewe anavyosema: “Haya, njoni, tusemezane… Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” Isa. 1:18.

“Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.” Isa. 43:25,26.

Je, ungependa kusemezana na kuhojiana na wakili huyu? Huna haja ya kumtafuta. Hivi sasa yuko katika mlango wa moyo wako (Ufu.3:20). Ukimfungulia sasa, ataingia na kuyabeba maovu yako yote na kukuwakilisha kwenye hukumu. Sasa hivi anabisha. Je, utamwacha aendelee kubisha bila kufungua mlango?

Je, utamkiri sasa mbele ya watu ili na yeye akukiri mbele ya Baba yake katika hukumu?