Yachunguzeni Maandiko Somo la 02 – Uovu Ulitoka Wapi?

Adamu na Hawa walikuwa wamesimama kando ya maiti ya mtoto wao wakilia. Muda mfupi kabla ya hapo, alikuwa amejaa furaha na uzima. Sasa alikuwa amekuwa mhanga wa muuaji. Kwa sababu ya hasira kali na wivu, ndugu yake mwenyewe aliinua silaha iliyoleta msiba katika familia ya kwanza kabisa hapa duniani.

Hawa angeweza kuuliza swali lile lile ambalo kina mama wengi wamekuwa wakiuliza. “Kwa nini Mungu? Kwa nini jambo kama hili limtokee mtu mwema kiasi hiki asiye na hatia? Lakini Hawa angeweza kuelezea vizuri zaidi sababu ya janga kama hilo kuliko mama mwingine ye yote, kwani wimbi la matatizo, ugonjwa na kifo lilitokana na uasi wake.

Sitaisahau siku ambayo mama yangu alikufa. Nilipofka nyumbani mwili wake ulikuwa umeshapelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti. Kila mmoja kati ya sisi watoto alikuwa ameshtuka. Kisha nikaenda kumtafuta baba yangu. Nilimkuta chumba cha chini akiwa analia na kuuliza, “Kama Mungu ni mwema hivyo, anawezaje kumchukua mama anayehitajiwa sana na watoto wake saba?”

Swali hilo lilidumu kichwani mwangu kwa miezikadhaa nikiwa natafuta jibu. Nililipata jibu katika Biblia, naningependa kuku eleza juu ya jibu hilo katika somo hili.

1. Dhambi ilianzia kwa nani?

“Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo.” 1Yoh. 3:8.

“Yule … nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani.” Ufu. 12:9.

Shetani aitwaye pia Ibilisi ndiye mwanzilishi wa dhambi. Bila ya Maandiko, chanzo cha uovu kisingejulikana.

2. Shetani alikuwa akiitwa nani kabla ya kuasi? Alikuwa akiishi wapi?

“Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe Nyota ya Alfajiri, mwana wa asubuhi!” Isa. 14:12.

“Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.” Luka 10:18. “Ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu.” Eze. 28:14.

Shetani alikuwa akiishi mbinguni alipoasi. Jina lake alikuwa Lusifa, yaani, “Nyota ya Alfajiri”.

3. Lusifa alitoka wapi? Alikuwa na cheo gani? Biblia inamwelezeaje?

“Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye.” Eze. 28:14. “Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri… Kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako… kazi ya matari yako na flimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari… Ulikuwa mkamilifu katika njia zako, hata uovu ulipoonekana ndani yako.” Eze. 28:12-15.

Lusifa alikuwa malaika aliyeumbwa na Mungu. Alikuwa mkamilifu katika hekima na uzuri na alisimama karibu na kiti cha enzi cha Mungu.

4. Ni jambo gani lililotokea katika maisha ya Lusifa lililomfanya aasi? Kisha alifanya dhambi gani ya kukufuru?

“Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako.” Eze. 28:17. “Nawe ulisema moyoni mwako… Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami… Nitafanana na yeye Aliye juu.” Isa. 14:13,14.

Kiburi, wivu, kutokuridhika na kujiinua nafsi viliinuka katika maisha yake. Lusifa aliamua kumwondoa Mungu katika kiti chake cha enzi na kudai kuwa yeye ndiye aabudiwe. Ulikuwa ni uhaini wa hali ya juu kabisa.

5. Kulitokea nini mbinguni baada ya Lusifa kuasi?

“Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.” Ufu. 12:7-9.

Kutoridhika kwa Lusifa, kulizaa uasi wa wazi dhidi ya Mungu. Theluthi ya malaka wa mbinguni waliungana naye katika jaribio la kumpindua Mungu. Matokeo yake Lusifa na wafuasi wake walitupwa kutoka mbinguni. 

6. Makao makuu ya Shetani kwa sasa yako wapi? Ana hisia gani juu ya wanadamu?

“BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi?

Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.” Ayu. 2:2. “Ole wa nchi na bahari! kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.” Ufu. 12:12. “Mshitaki wenu ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”

Makao makuu ya Shetani ni duniani na siyo Jehanum kama wengi wanavyofkiria. Anawachukia wanadamu na lengo lake ni kumwumiza Mungu kwa kukuangamiza wewe.

7. Mungu aliwazuia Adamu na Hawa kufanya jambo gani? Adhabu yao ilikuwa nini kama wasingetii?

“Walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.” Mwa. 2:17.

Adamu na Hawa hawakupaswa kula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, na adhabu yake ilikuwa ni kifo kama wangeasi.

8. Je, kula kipande cha tunda lilikuwa jambo baya kiasi hicho?

Kwa nini Adamu na Hawa waliondolewa katika Bustani ya Edeni?

“Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi.” Yak. 4:17. “Dhambi ni uasi.” 1 Yoh. 3:4. “Atendaye dhambi ni wa Ibilisi.” 1 Yoh. 3:8.

“BWANA Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele.” “Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.” Mwa. 3:22,24.

Kula tunda walilokatazwa kuliwafanya Adamu na Hawa kuwa washirika wa Shetani, ambaye ni adui mkuu wa Mungu.

9. Je, Biblia hufunua mambo gani ya ajabu juu ya mbinu za Shetani katika kuumiza, kudanganya, kukatisha tamaa na kuangamiza watu wa Mungu?

Shetani hutumia kila mbinu inayoweza kufkirika kuwadanganya na kuwaharibu watu. Mapepo wake wanaweza kuonekana kama watu wenye haki, na hata kama Wachungaji.

Biblia Inasema Shetani

 

Hudanganya/hutesa Ufu. 12:9,13  Hunukuu/hupotosha Biblia Mat.4:5,6
Husingizia/Huua Ufu. 12:10; Yn 8:44   Hutega/huvizia 2Tim. 2:26;
1 Pet. 5:8
Hufanya vita na watu wa Mungu Ufu. 12:17  Hufunga/huchochea usaliti Lk. 13:16; Yn 13:2,21
Hutia Gerezani Ufu. 2:10   Huwaingia watu/huzuia
Lk. 22:3-5; 1 The. 2:18
Hufanya miujiza/uongo Ufu. 16:13,14; Yn 8:44   Hujifanya malaika wa nuru
2 Kor. 11:13-15
Huleta magonjwa/maumivu Ayu. 2:7 Mapepo wake hujifanya wachungaji 2 Kor. 11:13-15
Ni mzushi “Ibilisi” maana yake ni mzushi. Huita moto toka mbinguni Ufu. 13:13

 

 

 

10. Je, majaribu na mikakati ya Shetani ina uwezo na mafanikio kiasi gani?

Aliwashawishi theluthi ya malaika (Ufu. 12:3-9). Adamu na Hawa (Mwa. 3); watu wote kasoro wanane katika siku za Nuhu (1 Pet. 3:20). Atawafanya waliopotea wajisikie wako salama (Mt. 7:21-23). Karibu dunia nzima itamfuata (Ufu. 13:8). Ni wachache watakaookolewa (Mt. 7:14; 22:14).

Nguvu ya udanganyifu wa Shetani katika siku za mwisho itakuwa kubwa kiasi kwamba karibu dunia nzima itamfuata.

11. Je, Ibilisi atapata lini na wapi adhabu yake? Adhabu yake itakuwa nini?

“Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia. Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto.” Mt. 13:40-42. “Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti.” Ufu. 20:10. “Ondokeni kwangu, mliolafaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake.” Mt. 25:41. “Basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao… wala hutakuwapo tena hata milele.” Eze. 28:18,19.

Mwisho wa dunia, Shetani atatupwa katika ziwa la moto ambao utamfanya kuwa majivu na kukomesha kuwepo kwake milele.

12. Ni jambo gani litakalomaliza tatizo baya la dhambi? Je, dhambi itainuka tena?

“Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; na kila ulimi utamkiri Mungu.” Rum. 14:11. (Soma pia Flp. 2:10,11; Isa. 45:23.) “Mateso hayatainuka mara ya pili.” Nah. 1:9.

Mambo mawili muhimu yatamaliza tatizo la dhambi. Kwanza, Viumbe vyote, mbinguni na duniani, pamoja na Ibilisi na malaika zake, kwa hiari yao wenyewe watapiga magoti na kukiri hadharani kuwa Mungu ni mkweli, asiye na upendeleo, na mwenye haki. Hakuna swali litakalobaki bila kujibiwa. Waovu wote watakiri wazi kuwa wamepotea kwa sababu waliukataa kwa ukaidi upendo na wokovu wa Mungu. Watakiri kwamba ili haki itendeke ni lazima wafe. Wote watakiri kwamba wanastahili mauti ya milele.

Pili, Dhambi itaondolewa ulimwenguni kwa kuteketezwa kabisa kwa dhambi, wenye dhambi, Ibilisi na malaika zake. Mungu yuko thabiti katika jambo hili: Dhambi haitainuka tena kuuchafua ulimwengu wa Mungu.

13. Ni nani anayefanya kuondolewa kabisa kwa dhambi ulimwenguni kuwa jambo la uhakika?

“Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” 1 Yoh. 3:8. “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi.” Ebr. 2:14.

Kwa njia ya maisha yake, kifo chake na kufufuka kwake, Yesu alifanya kuondolewa kwa dhambi liwe jambo la uhakika.

14. Je, Mungu Baba ana hisia gani juu ya watu?

“Kwa maana Baba mwenyewe awapenda.” Yn 16:27. (Soma pia Yn 3:16; 17:22,23.)

Baba anawapenda watu kama vile Mwana awapendavyo. Kusudi kubwa la Yesu lilikuwa kudhihirisha tabia ya Baba yake katika maisha yake ili watu wajue jinsi alivyo na upendo, mchangamfu, na mwenye kujali. “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile” (Yn 5:19).

Shetani amezua uongo mwingi kuhusu tabia ya Baba, kwamba hajali, ni mwenye sheria kali, mkali na asiyeingilika (ambazo ni tabia zake yeye mwenyewe). Hata matendo yake mabaya katika majanga huyaita “kazi ya Mungu”. Yesu alikuja kufuta uzushi huu na kuonyesha kuwa Baba yetu wa mbinguni anatupenda zaidi ya mama apendavyo mtoto wake. “Je! mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe” (Isa. 49:15). Somo kuu la Yesu lilikuwa uvumilivu wa Mungu, upole na rehema tele. Baba anasubiri kwa hamu, ili kuwafanya watu wawe na furaha kuu, Baba yetu wa mbinguni, amewaandalia makao mazuri ajabu! Ndoto zetu haziwezi kulingana na yale yanayotungojea! Anasubiri kwa hamu kuwakaribisha watu wake siku ile ya furaha ya kurejea nyumbani ambayo i karibu sana. Tunapaswa kuitangaza mbiu hii. Na tuwe tayari. Tuko katika siku za mwisho.

Baba anakupenda kama vile Yesu anavyokupenda. Je, unadhani kwamba hii ni habari njema?

Kama hii ni habari njema kwako, je, utamruhusu sasa Mungu atimize mapenzi yake katika maisha yako, kwa kujifunza na kuyafanya mapenzi yake kama yalivyo katika Biblia?