Yachunguzeni Maandiko Somo la 10 – Miaka 1000 Ya Amani

Nilimsikia mtu mmoja akisema hivi karibuni, “Sasa hivi Shetani amefungwa, tuko ndani ya ile miaka 1000.” Mchungaji alimjibu, Bila shaka amefungwa kwa mnyororo wa mpira wenye urefu toka Paris hadi Bombay, na kutoka Washington hadi Moscow.

Lakini tukiangalia mambo yanayotokea sasa hivi tunaweza kujua wazi kabisa kwamba Ibilisi bado yuko huru. Shughuli zake kwa sasa zimepamba moto kuliko wakati mwingine wo wote ule. Lakini hivi karibuni shughuli zake zitasitishwa kabisa. Hataweza kumjaribu, kumtesa, kumwangamiza ye yote katika watoto wa Mungu. Ibilisi atakuwa amefungwa.

Kipindi hiki ni cha miaka 1000. Maneno haya “miaka elfu moja” yanapatikana mara sita katika Ufunuo 20. Kuna dhana nyingi juu ya miaka hii 1000. Lakini Biblia inaeleza wazi jinsi miaka hiyo itakavyoanza, madhumuni yake na jinsi itakavyokwisha. Kabla ya kuanza somo hili, soma Ufunuo 20 yote.

1. Ni tukio gani litakaloashiria mwanzo wa hiyo miaka 1000?

“Nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya Neno la Mungu … nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.” Ufu. 20:4.

Ufufuo utakuwa ndiyo mwanzo wa miaka 1000.

2. Ufufuo huo unaitwaje? Ni akina nani watakaofufuliwa katika ufufuo huo?

“Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza.” Ufu. 20:5,6.

Unaitwa ufufuo wa kwanza. Wenye haki watafufuliwa katika ufufuo wa kwanza. Ufufuo wa wenye haki ndio utakaoanzisha miaka 1000.

3. Biblia inasema kutakuwa na ufufuo wa aina mbili. Ufufuo huu mwingine utatokea lini, na ni akina nani watafufuliwa katika ufufuo huo?

“Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.” Ufu. 20:5. “Watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.” Yn 5:28,29.

Ufufuo mwingine utatokea mwishoni mwa ile miaka 1000. Waovu watafufuliwa katika ufufuo huo. Unaitwa ufufuo wa hukumu. Tafadhali zingatia: Ufufuo wa wenye haki utaanzisha miaka 1000. Ufufuo wa waovu utahitimisha miaka 1000.

4. Tukio gani jingine la muhimu litatokea wakati miaka 1000 inaanza?

“Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona.” Ufu. 1:7. “Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko,… nao waliokufa katika Kristo watafufuka kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani.” 1 Thes. 4:16,17. “Palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo.” “Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena. Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta” [makadirio ya wasomi yanatofautiana kuanzia ratili 58 hadi 100]. Ufu. 16:18,20,21. (Angalia pia Yer. 4:23-26; Isa. 24:1,3,19,20; Isa. 2:21.)

A. Yesu atakuja katika mawingu (Ufu. 1:7).

B. Wenye haki waliofufuliwa na walio hai watanyakuliwa kumlaki Bwana hewani.

C. Tetemeko kuu pamoja na mvua ya mawe.

5. Waovu watakaokutwa wako hai watafanywa nini?

“Kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.” Isa. 11:4. “Wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake; katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu.” 2 Thes. 1:7,8. “Kama moshi upeperushwavyo, ndivyo wapeperushwavyo wao, kama nta iyeyukavyo ndani ya moto, ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu.” Zab. 68:2. “Na waliouawa na BWANA siku ile watakuwapo, toka upande mmoja wa dunia hata upande wa pili; hawataliliwa, wala kukusanywa, wala kuzikwa; watakuwa samadi juu ya uso wa nchi.” Yer. 25:33. “Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.” Ufu. 20:5.

Waovu watauawa mbele za Bwana. “Watakuwa samadi juu ya uso wa nchi.”

6. Je, waovu watakaokutwa wamekufa watakwenda wapi?

“Hao wafu waliosalia [waovu] hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.” Ufu. 20:5.

Watabaki katika makaburi yao hadi mwisho wa ile miaka 1000.

7. Hali ya dunia itakuwaje wakati wa miaka 1000?

“Naliiangalia nchi, na tazama, ilikuwa ukiwa, haina watu; naliziangalia mbingu, nazo zilikuwa hazina nuru.” “Nikaangalia, na tazama, hapakuwa na mtu hata mmoja, na ndege wote wa angani wamekwenda zao.” “Maana BWANA asema hivi, Nchi yote itakuwa ukiwa; lakini sitaikomesha kabisa.” Yer. 4:23,25,27. “Dunia hii itafanywa tupu kabisa, na kuharibiwa kabisa; maana BWANA amenena neno hilo.” Isa. 24:3.

Dunia itakuwa ukiwa, tupu, giza. Haitakuwa na mtu. Itakuwa imejaa mizoga ya waovu. Uvundo!

Kuna watu wanaoamini kuwa waovu watapata nafasi ya kutubu wakati wa miaka 1000. Si kweli. Hakutakuwa na mtu duniani! Watakuwa mizoga, na wenye haki watakuwa mbinguni!

8. Biblia inasema Shetani atafungwa Kuzimu. Kuzimu ni wapi?

“Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya Mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.” Ufu. 20:1-3.

Neno lililotafsiriwa “kuzimu” ni neno la Kigiriki “abussos.” Limetumika pia katika Mwa. 1:2 inapoelezea hali ya dunia ilivyokuwa kabla ya kuwepo kwa viumbe hai. “Nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu.” Hivyo kuzimu hapa linamaanisha dunia iliyo ukiwa na tupu. Itakuwa kuzimu kweli. Mizoga na mifupa ya waovu imeenea kila mahali. Dunia hii itakuwa jela ya Shetani kwa miaka 1000.

9. Na mnyororo unaomfunga ni nini? Kwa nini afungwe?

Mnyororo ni ishara – Mnyororo wa mazingira. Shetani ni roho, na roho haiwezi kufungwa kwa mnyororo wa kawaida. Shetani atakuwa amefungwa kwa sababu hatakuwa na watu wa kuwadanganya. Waovu watakuwa wamekufa wote, na wenye haki watakuwa mbinguni.

10. Wakati wa miaka 1000 watakatifu watakuwa wanafanya nini kule mbinguni?

“Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya Neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao. Wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.” Ufu. 20:3. “Au hamjui ya kwamba watakatifu tutauhukumu ulimwengu?… Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika…?” 1 Kor. 6:2,3.

Watakatifu wote watashiriki katika hukumu wakati wa miaka 1000. Taarifa za waliopotea pamoja na za Ibilisi na malaika zake zitapitiwa tena. Hukumu hii itaweka wazi taarifa za wote waliopotea. Hatimaye, kila mtu ataona kuwa amepotea kwa sababu hakupenda kuishi kama Yesu au kuwa pamoja naye.

Wakati wa miaka 1000 kila binadamu aliyewahi kuishi atakuwa kwenye moja ya sehemu hizi mbili:

1) Duniani, akiwa amekufa na kupotea, au

2) Mbinguni akishiriki katika hukumu.

11. Mwishoni mwa miaka 1000, Mji Mtakatifu, Yerusalemu Mpya, utashuka toka mbinguni. Ni akina nani watakuwa katika mji ule? Utatua wapi?

“Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu Mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu… Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.” Ufu. 21:2,3. “Tazama, siku moja ya BWANA inakuja, ambayo mateka yatagawanyika kati yako… Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya Mlima wa Mizeituni… utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini… BWANA, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye… Na watu watakaa ndani yake, wala hakutakuwako laana tena, lakini Yerusalemu utakaa salama.” Zek. 14:1,4,5,11.

Yerusalemu Mpya utatua mahali ulipo Mlima wa Mizeituni kwa sasa. Mlima utasawazishwa kufanya uwanda mkubwa ambapo mji utatua. Wenye haki wote (Zek. 14:5), malaika wa mbinguni (Mt. 25:31), pamoja na Mungu Baba (Ufu. 21:2,3) na Mungu Mwana (Mt. 25:31) watarejea duniani wakiwa katika mji mtakatifu wakati Yesu atakapokuja mara ya tatu. Mara ya pili atakuja kuwachukua watakatifu wake. Mara ya tatu atakuja pamoja na watakatifu wake.

Kuja kwa Yesu
A. Mara ya kwanza, Bethlehemu, kwenye hori la ng’ombe.
B. Mara ya pili, katika mawingu mwanzo wa miaka 1000.
C. Mara ya tatu, katika Mji Mtakatifu pamoja na watakatifu mwishoni mwa miaka 1000.

12. Atakapokuja mara ya tatu waovu waliokufa watafanyiwa nini? Jambo hilo litamaanisha nini kwa Shetani?

“Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.” “Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake; naye atatoka kuwadanganya Mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.” Ufu. 20:5,7,8.

Waovu watafufuliwa baada ya miaka 1000 kuisha. Shetani atapata tena watu wa kuwadanganya na kwa njia hiyo atakuwa ametoka kifungoni kwake na kuwadanganya tena Mataifa.

13. Shetani atachukua hatua gani?

“Naye atatoka kuwadanganya Mataifa walio katika pembe nne za nchi.” “Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu.” Ufu. 20:7-9.

Ataanza kuwadanganya tena waovu waliofufuliwa. Atawadanganya kuwa kama wakishirikiana naye wanaweza kuuteka ule mji wa watakatifu. Hivyo Mataifa watakusanyika na kuuzingira ule mji.

14. Jambo gani litakatisha mipango ya Shetani?

“Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala. Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika lile ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo.” Ufu. 20:9,10. “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.” Ufu. 21:8. “Watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza… haitawaachia shina wala tawi.” “Nanyi mtawakanyaga waovu; maana watakuwa majivu chini ya nyayo za miguu yenu.” Mal. 4:1,3.

Moto utashuka ghafula toka Mbinguni – (siyo kutoka Jehanum kama wengi wanavyoamini) – juu ya waovu na wote watafanywa kuwa majivu, pamoja na Shetani na malaika zake. Mt. 25:41; Eze. 28:17-19.

Moto huu utawateketeza waovu kabisa. Hii inaitwa mauti ya pili. Moto huu utakapokuwa umeteketeza kila kitu, hatimaye utazimika.

15. Lakini mbona unaitwa moto wa milele?

“Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiangamizwa katika moto wa milele.” Yuda 7.

Hata moto uliounguza Sodoma na Gomora unaitwa wa milele, lakini ulishazimika karne nyingi zilizopita (2 Pet. 2:6).

16. Je, Biblia haisemi kuwa wataadhibiwa milele?

Neno ‘milele’ mara nyingi linamaanisha“hadi kufa” au “maisha yake yote.”

Katika 1 Nya. 28:4 Daudi alisema, Bwana”alinichagua kuwa mfalme wa Israeli milele.” Lakini Daudi alikuwa mfalme hadi alipokufa tu.

Mithali 29:14 inasema, “Mfalme awahukumuye maskini kwa uaminifu, kiti chake cha enzi kitathibitika milele.” Lakini wafalme wote wema viti vyao vya enzi leo havipo! Kwa hiyo, moto wa milele utawateketeza Ibilisi pamoja na watu wake hadi kufa! Kwa maana “Mshahara wa dhambi ni MAUTI” (Rum. 6:23). Na siyo UZIMA WA MILELE kwenye moto.

17. Baada ya waovu kuteketezwa na moto kuzimika, tukio gani la utukufu litatokea?

“Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.” Isa. 65:17. “Lakini, kama ilivyo ahadi yake, tunatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake.” 2 Pet. 3:13. “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya… Maneno hayo ni amini na kweli.” Ufu. 21:5. “Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.” Ufu. 21:3.

Mungu atafanya mbingu mpya na nchi mpya na Yerusalemu Mpya itakuwa makao makuu ya nchi mpya.

18. Je, tunaweza kujua mwanzo wa miaka 1000 ulivyokaribia?

“Nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni.” Mt. 24:33. “Basi mambo hayo yaanzapo kutokea, changamkeni, mkaviinue vichwa vyenu, kwa kuwa ukombozi wenu umekaribia.” Lk. 21:28. “Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.” 1 Thes. 5:3.

Yesu alisema tukiona dalili za kuja kwake zinatimia upesi, kama tunavyoona leo, tushangilie na kujua kuwa kuja kwake ku karibu. Mtume Paulo pia anatuambia kuwa tukiona vuguvugu la kutafuta amani duniani tujue kuwa kuja kwake kumekaribia. Ni hakika kuwa muda umekwisha. Bwana atakuja ghafula katika saa asiyotegemea mtu (Mt. 24:36). Njia pekee ni kuhakikisha kuwa tuko tayari.

Yesu, aliyekupenda kiasi cha kuja kuishi kama mwanadamu na kufa kwa ajili ya dhambi zako, amekuandalia makao katika mji mpya wa Yerusalemu. Na hivi karibuni atakuja kuwachukua waliokubali kwenda kuishi na kutawala naye hiyo miaka 1000.

Je, unafanya mipango ya kwenda pamoja naye kuishi katika nyumba ya utukufu ambayo Yesu mwenyewe amekuandalia?