Somo 23 JEHANAMU NI NINI NA IKO WAPI?

JEHANAMU NI NINI NA IKO WAPI?

Kufyatua risasi kipumbavu kulitokea wakati mwanafunzi mmoja alipoingia katika shule yake na kuwaua wanafunzi wenzake kadhaa. Mwanaume mmoja mwenye chuki, ambaye alikuwa amefukuzwa kazi, aliingia mahali pale alipokuwa akifanya kazi zamani na kumpiga risasi mkuu wake wa kazi. Mama mmoja alisukuma gari lake dogo na kulitumbukiza ziwani likiwa na watoto wake wawili ndani yake na kuwazamisha.

Kwa uchache katika mabara mawili maelfu wamechinjwa katika mauaji ya safisha-safisha ya kikabila. Uhasama wa muda mrefu uliochukua karne nyingi kati ya makundi mawili au zaidi ya makabila hayo ndicho chanzo chake. Wanaume, wanawake, watoto, na hata watoto wachanga wamepigwa risasi, wamekatwa-katwa, wamepigwa, na kubakwa.

Kutoa adhabu ya kifo kwa uhalifu huo wa kishenzi, hata kwa wauaji wale walio wakatili sana, kunashutumiwa na wengi. Makundi yaliyo kinyume na hukumu ya kifo yanapinga kwa makelele mengi, wakiita hukumu hiyo kuwa sio ya kibinadamu ati ni “mfumo wa ibada ya kipagani.” Wanauliza hivi, je! wauaji hao hawarekebishiki?

Je! njia sahihi ya kibinadamu ya kuwaua wahalifu waliohukumiwa kuuawa ni ipi? Je! ni kile kiti cha umeme? Wengine wanadhani kudungwa sindano yenye sumu ya kufisha ingekuwa ni njia isiyo na maumivu kabisa. Wengine wanatetea kwamba uhai wa mtu ungekoma kwa upesi zaidi kwa kumnyonga.

Lakini, basi Wakristo wengi waaminifu wanadhani kwamba Baba yetu aliye mbinguni atatenda vibaya kuliko hivyo. Wao wanasema, waovu ni lazima wateswe vibaya ili kubatilizwa kwa ajili ya dhambi zao. Tena, zaidi sana ya hayo, wanafikiria kwamba maeneo ya Mungu anayoyatumia kuwaulia wahalifu ni mahali pa mateso yasiyo na mwisho.

Ni kitu gani hasa kinachowapata waovu? Je! maangamizi yao yanapatanaje na upendo na haki ya Mungu? Hebu na tuangalie Biblia itupe jibu.

1. Huzuni Kubwa Ya Mwisho Ya Yesu

Kwa miaka 6,000 Mungu amekuwa akiwasihi sana wanaume na wanawake:
“Kama mimi niishivyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu…mimi sikufurahii kifo cha mtu mwovu, bali napenda mtu mwovu aachane na mwenendo wake mbaya, apate kuishi” – (Ezekieli 33:11).

Msalaba ulidhihirisha ni kwa kiwango gani Mungu anataka kuwaokoa wanadamu walioanguka [dhambini]. Yesu alipopaza sauti pale msalabani, akisema, “Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo,” aliufunua wazi moyo wake uliokuwa ukimwuma (Luka 23:34). Muda mfupi baada ya hapo Yesu akakata roho, na kama wengine waaminivyo, akafa kwa kupasuka moyo wake (Yohana 19:30, 34).

Lakini hata pamoja na udhihirisho huo wenye nguvu ya upendo wa Mungu, watu wengi bado hawamgeukii Yesu. Na kadiri dhambi inavyoendelea kutawala katika dunia hii, ndivyo itakavyozidi kuongeza misiba ya wanadamu. Kwa hiyo ni lazima dhambi iteketezwe kabisa. Je! hivi Mungu anapanga kufanya nini ili kuikomesha hiyo dhambi?

“Siku ya Bwana itakuja…. mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; na vitu vyake vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia itatoweka…” – (2 Petro 3:10).

Hatimaye ni lazima Mungu aitakase dunia hii kutokana na uovu wake na kuikomesha dhambi kabisa. Wale wanaoendelea kung’ang’ania dhambi hatimaye watateketezwa kwa moto huo ulioandaliwa kwa ajili ya kumteketeza Iblisi, malaika zake, na dhambi katika dunia yetu hii. Ni wakati wa kuhuzunisha jinsi gani kwa Yesu anapouangalia moto ukiwateketeza wale aliokuja kuwafia ili kuwaokoa.

2. Wapi Na Lini Utakapowaka Moto Wa Jehanamu?

Kinyume na dhana zinazopendwa sana na watu wengi, Mungu hana moto unaowaka sasa mahali paitwapo “jehanamu” ambapo wafu huenda wanapokufa. Jehanamu hutokea wakati ule dunia hii itakapogeuka na kuwa ziwa la moto. Mungu anangojea kutekeleza hukumu hiyo dhidi ya waovu mpaka hapo hukumu ya mwisho itakapotolewa mwisho wa ile miaka 1,000 (Ufunuo 20:9-15).

“Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa katika majaribu watu wanaomcha Mungu, na jinsi ya kuwaweka waovu katika adhabu hadi siku ile ya hukumu” – (2 Petro 2:9).

Pia anaitakasa dunia yetu kwa moto huo utakasao.

“Lakini Mbingu na nchi za sasa zimehifadhiwa kwa neno la Mungu kwa ajili ya kuharibiwa kwa moto. Zimewekwa kwa ajili ya siku ile ambapo watu wasiomcha Mungu watahukumiwa na kuangamizwa.” – (2 Petro 3:7).

Kamwe Mungu hakupanga kwamba mwanadamu awaye yote amalizie maisha yake katika mioto ile ya jehanamu. Lakini watu wanapokataa katakata kuachana na Shetani, halafu wanaendelea kuzing’ang’ania dhambi zao, basi, ni lazima wapokee hatimaye matokeo ya uchaguzi wao.

“Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! nedeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake” Mathayo 25:41.

Kulingana na maneno hayo ya Kristo, je! ni lini jehanamu itakapowaka moto?

“Kama vile magugu yanavyokusanywa na kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwisho mwa nyakati; Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu, na kuwatupa katika tanuru ya moto, na watalia na kusaga meno. Kisha, wale wema watang’ara kama jua katika ufalme wa Baba yao. mwenye masikio na asikie!” – (Mathayo 13:40-42).

Magugu, yaani, wale watendao maovu, hawachomwi moto mpaka utakapofika ule mwisho wa dunia. Kabla haijatekelezwa hiyo hukumu, malimwengu yote hayana budi kuthibitisha kwamba Mungu ni mwenye haki katika kumshughulikia kila mwanadamu. Kama ilivyoelezwa kwa kinaganaga katika Somo la 22, katika pambano kuu linaloendelea kati ya Kristo na Shetani, Shetani amekuwa akijaribu kuyathibitishia hayo malimwengu kwamba njia ya dhambi ndiyo njia bora; Yesu amekuwa akionyesha wazi kwamba njia ya utii ndiyo ufunguo wa maisha yanayoridhisha zaidi.

Mwisho wa miaka ile 1,000, udhihirisho huo utaishia katika hukumu ya Shetani, malaika zake, na waovu. Baada ya kufunguliwa vitabu vya kumbukumbu ambavyo vinafichua sehemu aliyofanya kila mtu katika mfululizo wa matukio hayo ya kusisimua, ndipo Mungu atakapomtupa Shetani, mauti na kaburi [kuzimu], pamoja na kila mmoja ambaye jina lake “halikuonekana limeandikwa katika kitabu cha uzima…. Katika ziwa la moto” (Ufunuo 20:15). Kulingana na fungu hili lifuatalo, yaani, Ufunuo 21:1, baada ya Mungu kuitakasa nchi hii kwa moto kutokana na dhambi, anaumba, “mbingu mpya na nchi mpya.”

3. Jehanamu Itawaka Kwa Muda Gani?

Waumini wengi wanalikubali wazo hili lisemalo kwamba mioto ile ya jehanamu inawaka milele na milele. Hebu na tuangalie kwa makini mafungu yale yanayoeleza jinsi Mungu anavyoishughulikia dhambi pamoja na wenye dhambi.

“Na miale ya moto huwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari njema ya Bwana ya Yesu. Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu” – (2 Wathesalonike 1:8,9).

Tafadhali zingatia kwamba hayo “maangamizi ya milele” sio sawa na “mateso makali ya milele.” Maana yake tu ni kwamba hayo ni maangamizi yanayoendelea milele. Matokeo yake ni mauti ya milele. Petro alizungumza juu ya siku ya hukumu na ya “kuangamizwa kwao wanadamu wasiomcha Mungu” (2 Petro 3:7).

Kulingana na Yesu, maneno yote mawili, yaani, “roho na mwili” huangamizwa katika Jehanamu (Mathayo 10:28). Katika hotuba yake ya
mlimani, Yesu alizungumza juu ya mlango ulio mwembamba “uendao uzimani,” na njia ile pana “iendayo kwenye maangamizi” (Mathayo 7:13,14). Katika Yohana 3:16, Yesu anaeleza kwamba Mungu “akamtoa Mwanawe pekee,” bali wawe na uzima wa milele.” Yesu anailinganisha miisho miwili: uzima wa milele au kuangamia sio kuchomwa moto milele na milele.

Tunapaswa kuhitimisha kwa kusema kwamba ni dhahiri ya kuwa jehanamu ina mwisho wake; mwisho wake ni mauti na maangamizi ya waovu.

Semi zinazoeleweka wazi katika maandiko yote zinatuambia kwamba waovu wataangamizwa. “Waovu wataharibiwa” (Zaburi 37:28), “wataangamizwa” (2 Petro 2:12), “watatoweka kama moshi” (Zaburi 37:20). Moto ule utawateketeza kabisa hadi watakuwa majivu (Malaki 4:1-3).
“Mshahara wa dhambi ni mauti, “sio uzima wa milele katika jehanamu; (Warumi 6:23).

Kusudi la adhabu ya mwisho katika moto ule wa jehanum ni kuiondoa dhambi kabisa ulimwenguni humu, sio kuiendeleza dhambi milele na milele. Ni vigumu kabisa kumwazia Kristo aliyeulilia mji ule mkaidi kutokana na ajali yake, na ambaye aliwasamehe wale waliomwua, kwamba atumie umilele wake wote kuyaangalia maumivu yale makali ya waliolaaniwa.

Ni dhahiri kwamba jehanamu ina mwisho wake. Mwisho wa miaka 1,000, Mungu ananyesha moto chini kutoka mawinguni na kumwangamiza kabisa Ibilisi, malaika zake, pamoja na waovu wanaoendelea kuzing’ang’ania dhambi zao. “Moto” huo una”shuka kutoka mbinguni” na kuwateketeza kabisa (Ufunuo 20:9).

Kulingana na maneno yake Kristo, moto huo ni “moto usiozimika” (Mathayo 3:12). Hakuna zima moto iwayo yote iwezayo kuuzima mpaka umalize kazi yake ya kuteketeza kabisa.

Mungu anaahidi kwamba, kutokana na moto huo utakasao, yeye ataiumba “nchi mpya,” ambayo ndani yake “taabu zote zilizopita zitakuwa zimesahaulika,” na “sauti ya kuomboleza na kulia haitasikika tena ndani yake” (Isaya 65:16-19).

Ile ni siku ilioje! Kila chanzo kiletacho huzuni kubwa kitakuwa kimetoweka kabisa. Mungu atayafutilia mbali kabisa majeraha ya dhambi kutoka katika kila moyo, ndipo furaha yetu itakuwa imetimilika.

4. “Milele” Katika Maandiko

Katika Mathayo 25:41 Yesu anazungumza juu ya “moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake.” Je, neno hili “milele” linadokeza kwamba jehanamu hiyo ni ya milele? Yuda 7, anaeleza habari za Sodoma na Gomora kuwa “imewekwa kuwa mfano wa wale watakaopata adhabu yao katika ule moto wa milele.” Ni dhahiri kwamba miji ile haiendelei kuteketezwa kwa moto ule. Lakini moto wenyewe ULIKUWA wa milele kwa maana kwamba ulisababisha maangamizi ya kudumu.

Katika 2 Petro 2:6 tunasoma mara moja tena habari za moto wa milele. Lakini maandiko hayo pia huonyesha wazi kwamba Mungu “akaihukumu miji ya Sodoma na Gomora, akiiteketeza kabisa kwa moto na kuifanya majivu, akaifanya iwe mfano wa kile kitakachowapata wale wasiomcha Mungu.” Wale wasiomcha Mungu waliokuwa Sodoma na Gomora hawaendelei kupata maumivu makali; waliteketezwa kabisa kuwa majivu zamani sana. Na, hata hivyo, moto ule uliowateketeza ni “wa milele’ kwa kuangalia matokeo ya kazi yake – yaani, maangamizi yale ya kudumu. Milele maana yake ni adhabu ya kudumu, sio kuendelea tu kuadhibiwa.

Kwa kuwa kile kitabu cha Ufunuo kinatumia lugha ya mifano dhahiri kama ile, baadhi ya vifungu vyake vya maneno vimeeleweka vibaya. Kwa mfano, Ufunuo 14:11 husema maneno haya juu ya wale waliopotea, “moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele.” Maneno haya yanasikika kana kwamba ni mateso yasiyo na mwisho. Lakini, tena, hebu na tuliache Andiko kulitafsiri Andiko.

Yona na samaki kubwaKutoka 21:6 katika toleo la KJV huzungumzia habari za mtumishi kutobolewa sikio lake kama ishara ionyeshayo kwamba yeye angeendelea kumtumikia bwana wake “milele.” Katika mfano huu neno hili “milele” lingemaanisha kadiri uhai wa mtumishi yule ambavyo ungeendelea kuwapo. Yona, aliyekaa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la yule nyangumi (Mathayo 12:40), anatoa taarifa yake kwamba alikuwa ndani mle “milele” (Yona 2:6). Bila shaka zile siku tatu na lile giza lisilokuwa na matumaini kwake vilionekana kana kwamba ni milele.

Basi hatuna budi kuwa waangalifu kuelewa ni jinsi gani na lini maandiko yanapotumia lugha ya mafumbo, ya mashairi. Moshi ukipanda juu milele kutoka katika ziwa lile la moto ni njia dhahiri ya kuonyesha maangamizi ya milele. Ufunuo 21:8 hutuambia waziwazi kwamba ziwa lile linalowaka moto na kiberiti “ni mauti ya pili.” Jehanum ina mwisho wake. Waovu wanateketezwa kwa moto; yaani, wanaangamizwa kabisa.

5. Kwa Nini, Iweko Hiyo Jehanamu?

Hapo mwanzo Mungu aliiumba dunia hii ikiwa kamilifu. Lakini dhambi ikaja na kuleta misiba, uharibifu, na mauti. Kama jioni moja ungerudi nyumbani kwako na kuikuta nyumba yako imepekuliwa na kuharibiwa, je! ungeiacha katika hali ile milele? Hasha. Ungefagia takataka na uchafu, ungepasafisha mahali pale kabisa, na kuitupilia mbali samani [fanicha] iliyoharibiwa kiasi cha kutoweza kutengenezeka tena. Mungu atafanya vivyo hivyo. Ataushughulikia uharibifu na uchafuzi wa dhambi kwa mara moja tu, na kuiumba dunia mpya mahali pake. Kusudi la Mungu kuitakasa dunia hii kwa moto ni kutayarisha njia ya kupatikana dunia kamilifu kwa ajili ya kuishi ndani yake wale waliookolewa.

Lakini Mungu anakabiliwa na tatizo zito kwa sababu dhambi hiyo haikuharibu tu dunia hii, bali pia imewaambukiza watu. Dhambi iliharibu uhusiano wetu naye na kati yetu sisi kwa sisi. Wanadamu wanaedelea kusumbuliwa na watoto wanaoteswa, ugaidi, picha za wanawake walio uchi zinazoamsha ashiki, na maelfu ya kansa nyingine za kiroho. Siku moja Mungu atalazimika kuiangamiza dhambi kabisa, kwa sababu dhambi ndiyo inayowaangamiza watu. Tatizo la Mungu ambalo ni gumu kulitatua ni hili; jinsi gani akiteketeze kile kirusi cha dhambi kiletacho mauti kutoka katika dunia hii na wakati huo huo asiweze kuwaangamiza watu wote walioambukizwa nacho? Suluhisho lake lilikuwa ni lile lakukichukua kirusi hicho cha dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe; akairuhusu ile kansa ya dhambi kumwangamiza yeye kabisa pale msalabani. Matokeo yake ni haya:
“Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, naye atatusamehe dhambi zetu na KUTUSAFISHA UDHALIMU WOTE.” – (1 Yohana 1:9).

Mungu anampa bure kila mmoja suluhisho lake kwa hilo tatizo la dhambi. Lakini ukweli wa kusikitisha ni kwamba wengine wanaung’ang’ania ugonjwa huo wa dhambi kwa nguvu zao zote. Na Mungu hatatumia nguvu kuwalazimisha watu hao ili wapate kuichagua njia yake ya uzima wa milele. Wale wanaolikataa suluhisho lake hatimaye wataangamizwa kabisa pamoja na ugonjwa huo. Sababu ya kweli ya kuwako hiyo jehanamu ni hii:
“Kwa sababu mimi nilipoita ninyi hamkuitika, niliponena hamkusikia. Mlitenda yaliyo mabaya machoni pangu, mlichagua mambo nisiyoyafurahia mimi” – (Isaya 65:12).

Wakiwa wametengwa mbali na Yesu kwa uchaguzi wao wenyewe, waovu watagundua kwamba kumbe njia pekee iliyobaki kwao ni kukabiliwa na ile mauti ya milele.

6. Nini Gharama Ya Kupotea?

Ijapokuwa maandiko hayafundishi kwamba moto ule wa jehanamu unasababisha maumivu yasiyo na mwisho, yanatupa picha ya haraka kuonyesha ni jambo la kutisha jinsi gani kupotea. Waovu wataukosa uzima wa milele. Litakuwa ni jambo la kuogofya jinsi gani kutambua kwamba furaha ile ya kuishi milele pamoja na Mungu imeteleza mikononi mwao, ya kwamba hawatauonja kamwe uhusiano ule wenye furaha kamilifu na upendo milele hata milele.

Kristo alipoangikwa pale msalabani, dhambi za ulimwengu mzima zikimtenga na Baba yake, bila shaka alipata wale watakaopotea milele. Waovu wanapoliangalia lile giza jeusi, lenye ukiwa, mbele yao, wanaona tu
maangamizi yao ya milele. Hawana budi kufa bila kuwa na tumaini la kufufuliwa mara ya pili. Wakati huo huo wanaona jinsi walivyomsukumia mbali huyo Kristo mara kwa mara alipokuja karibu nao akiwa na maneno ya upendo ya kutaka kufanya amani nao. Mwisho watapiga magoti yao na kukiri kwamba Mungu ni mwenye haki na upendo (Wafilipi 2:10,11).

Si ajabu, basi, kwamba waandishi wa Biblia wanasisitiza sana juu yetu kuhusu uzito wa uchaguzi wetu tunaofanya pamoja na madai ya Kristo kwetu.

“Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure, Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia”. Basi, sasa ndio wakati wa kufaa, sasa ndiyo siku ya wokovu” – 2 Wakorintho 6:1,2.

Siwezi kufikiria juu ya msiba mkubwa kuliko ule wa mtu fulani anayeitumia vibaya kafara ya Yesu kwa kuchagua kupotea. Njia zilizobaki mbele yetu ziko dhahiri kabisa: yaani, yale maangamizi ya milele – kutengwa milele mbali na Mungu, au urafiki wa milele pamoja na Kristo ambao unakidhi shauku yetu ya ndani kabisa ya moyo wetu. Je! wewe unachagua ipi? Kwa nini wewe usiugundue mwisho wako kwa kukaa ndani ya Kristo leo?

© 2004 The Voice of Prophecy