Somo 22 JE! MUNGU ANA HAKI?

JE! MUNGU ANA HAKI?

Mvulana mmoja ndani kabisa ya mji anauawa kwa risasi zilizofyatuliwa ovyo na majambazi wakati anafanya kazi yake ya shuleni akiwa ameketi nyumbani kwao katika meza ya familia yake.

Mama mmoja kijana katika viunga vya mji anagundua kwamba mtoto wake amepatikana na Ukimwi kutokana na damu aliyoongezewa mwilini mwake.

Misiba inazidi kuendelea tena na tena katika ulimwengu wetu huu. Nasi tunatamani sana kujua jibu kwa mambo hayo yote. Hivi Mungu huyo yuko wapi katika ulimwengu wetu huu uliojaa mateso na vifo visivyo na maana? Mtunga Zaburi anatuhakikishia sasa kwamba ” dunia hii imejaa upendo wake usio na mwisho” (Zaburi 33:5).

Lakini, basi, kama hilo ni jambo la kweli, mbona hayakomeshi mateso hayo pamoja na misiba? Sura ya 20 ya Ufunuo inatuonyesha sisi ni kwa ajili gani na lini Mungu atakapo komesha dhambi na mateso.

1. Miaka Ile Elfu Moja Yafunuliwa

Ufunuo 20 huelekeza mawazo yetu yote kwenye kipindi kile cha miaka 1,000 ambacho kinakuja baada ya Kristo kuja mara ya pili. Matukio yale yanayokizunguka kipindi hicho cha mika 1,000 ni lile tendo la mwisho katika pambano ambalo limekuwa likiendelea kati ya Kristo na Shetani tangu dhambi ilipoingia katika ulimwengu huu.

Mfululizo wa matukio hayo ya kuvutia macho ulianza kule mbinguni wakati Lusifa alipomuonea wivu Kristo, akaanzisha vita kule dhidi ya malaika wale ambao hawakuanguka [dhambini] alifukuzwa kule, na kukimbilia katika dunia yetu. Matukio hayo yaliendelea hapa duniani katika ile Bustani ya Edeni, halafu kupitia katika Karne zote na kushuka hadi yalipofikia kilele chake cha kwanza wakati ule Ibilisi alipowachochea wanadamu kumsulibisha Kristo. (Ukipenda waweza kukipitia tena kisa hicho cha kusikitisha katika Somo la 3.) Matukio hayo yatafikia kilele chake cha mwisho kitakapokwisha kipindi kile cha miaka 1,000 wakati dunia yetu hii yenye dhambi itakapotakaswa na kuwekwa chini ya utawala wa Kristo. Ufunuo 20 unatuonyesha sisi kwamba kipindi hicho cha miaka 1,000 kimetenganishwa na ufunuo wa aina mbili.

Je! Ni akina nani hao ambao Mungu anawafufua kutoka kwa wafu katika ufufuo wa kwanza unaotokea mwanzo wa ile miaka 1,000?
“Wameneemeka sana, heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja”- (Ufunuo 20:6).

Wale walio “heri na watakatifu,” yaani, wale waliompokea Kristo kama Mwokozi wao wanatoka katika ule ufufuo wa kwanza wa wenye haki na hawana budi kutawala pamoja na Kristo katika kipindi cha miaka 1,000 basi, ni lazima wafufuliwe mwanzo wa ile miaka 1,000.

Je hao ni akina nani wanaofufuliwa katika ufufuo wa pili utakaotokea mwisho wa kipindi cha miaka elfu moja?

Hao wafu Waliosalia hawakuwa hai mpaka ilipokwisha ile miaka elfu moja – (Ufunuo 20:5).

Maneno haya “hao wafu waliosalia” yanaweza tu kuwataja waovu wale waliokufa kwa sababu wale wenye haki ambao ni heri na watakatifu wanaofufuliwa mwanzo wa ile miaka 1000.

Kwa hiyo, hicho kipindi cha miaka 1,000 kimetenganishwa na ufufuo wa aina mbali : yaani, ufufuo wa wenye haki unatokea mwanzo wake, na ufufuo wa waovu unaotokea mwisho wake.

2. Kufufuliwa Wakati Wa Marejeo Ya Kristo

Ufufuo wa kwanza, yaani, ule wa wenye haki unatokea wakati wa kuja mara ya pili kwa Kristo.

“Maana patatolewa amri, sauti ya tarumbeta ya Mungu, naye Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni. Ndipo wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai wakati huo tutakusanywa pamoja nao katika mawingu kumlaki Bwana hewani. Na hivyo tutakuwa daima pamoja na Bwana” (1 Wathesalonike 4:16,17).

Yesu anapokuja katika dunia hii anawafufua wale “waliokufa katika Kristo” na kuwachukua kwenda nao mbinguni pamoja na wenye haki wale walio hai. Kwa kuwa wale waovu bado wanaendelea kung’a ng’ania dhambi, hawawezi kuendelea kuwa hai mbele zake Mungu, nao wanaangamizwa wakati ule wa kuja kwake Kristo (Luka 17:26-30). (Unaweza kupenda kupitia tena Somo la 8 uhusuo matokeo yale yanayoambatana na kurudi kwa Yesu).

3. Shetani Afungwa Mnyororo Hapa Duniani Kwa Miaka Elfu Moja

Miaka hiyo elfu moja inapoanza, wenye haki wote watakuwa wamekwisha kwenda zao mbinguni, na waovu watakuwa wamekufa wote. Je! hivi kutatokea nini juu ya dunia hii katika hiki kipindi cha miaka 1,000?

“Kisha, nikamwona malaika mmoja anashuka kutoka mbinguni akiwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akalikamata lile joka – nyoka wa kale, yaani Ibilisi au Shetani – akalifunga kwa muda wa miaka elfu moja. Malaika akalitupa kuzimu, akaufunga mlango wa kuingilia huko na kuutia mhuri ili lisiweze tena kuyapotosha mataifa mpaka hapo miaka elfu moja itakapotimia. Lakini baada ya miaka hiyo ni lazima lifunguliwe tena, lakini kwa muda mfupi tu ” Ufunuo 20:1-3.

Wakati wa kuja kwake Yesu Shetani anafungwa, naye atabaki na minyororo yake katika kipindi kile cha miaka 1,000. Je! Ni wapi atakapofungwa Shetani? Atafungwa “kuzimu” (Abyss), hili ni neno la Kigiriki limaanishalo “kilindi kirefu” au “shimo la kuzimu” katika Mwanzo 1:2 tafsiri ya Kigiriki ya Agano la Kale inatumia neno hili “vilindi” (Abyss) kuielezea dunia hii ilipokuwa katika hali yake isiyotengenezwa vizuri kabla ya siku zile za uumbaji kuanza. Kwa hiyo dunia yetu hii ndiyo iitwayo kuzimu (Abyss), ni mahali ambapo Mungu anamfunga Shetani kuwa amefungwa “na minyororo halisi? La, ni mfano, ni mnyororo wa mazingira. Shetani angependa sana kuendelea kuwadanganya wanadamu katika kipindi kile cha miaka 1,000. Lakini, basi, yeye hawezi kuwapata wenye haki wowote wa kuwajaribu, kwa sababu wote wako kule mbinguni. Wala hawezi kuwapata waovu wa kuwaongoza, kwa kuwa wote wamekufa, wamelala usingizi wa mauti katika mavumbi ya ardhi. Akiwa hana uwezo wowote wa kuwadanganya au kuwajaribu, anatangatanga katika dunia hii tupu akilazimishwa kutafakari huzuni kubwa na misiba aliyoisababisha.

4. Wenye Haki Wanawahukumu Waovu

Kipindi kile cha miaka elfu moja ni kipindi cha hukumu pia. Lakini kumbuka kwamba hukumu hiyo ina hatua kuu nne:

(1) Hukumu ya wenye haki kabla ya kuja kwa Kristo mara ya pili.
(2) Thawabu ya wenye haki wakati ule wa kuja mara ya pili kwa Kristo.
(3) Hukumu ya waovu katika kipindi kile cha miaka elfu moja.
(4) Thawabu ya Shetani na waovu mwishoni mwa kipindi kile. (ukipenda waweza kuupitia tena Soma la 13 ambao unashughulika na hatua ya 1 na ya 2 ya hukumu hiyo, yaani, upelelezi na thawabu ya wenye haki.)

Tumekwisha kuona ya kwamba wenye haki waliokufa ambao wamekwisha kufufuliwa, pamoja na wenye haki wale walio hai wananyakuliwa kwenda mbinguni wakati ule wa kuja kwake Kriso mara ya pili. Wao wako nyumbani kwao kule mbinguni katika kipindi kile cha miaka 1,000. Je, watakuwa wakifanya nini huko?

“Je! hamjui kwamba watu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Ikiwa basi, ulimwengu utahukumiwa nanyi kwa nini hamstahili kuhukumu hata katika mambo madogo? hamjui kwamba, licha ya kuhukumu mambo ya kawaida ya kila siku, tutawahukumu hata malaika?” – (1 Wakorintho 6:2-3).

“Kisha nikaona viti vya enzi na watu walioketi juu yake; watu hao walipewa mamlaka ya hukumu. Niliona pia roho za wale waliokuwa wamenyongwa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. hawa hawakumwabudu yule mnyama na sanamu yake, wala hawakupigwa alama yake juu ya paji ya nyuso zao, au juu ya mikono yao. Walipata tena uhai, wakawatawala pamoja na Kristo kwa miaka elfu moja “- (Ufunuo 20:4).

Katika kipindi kile cha miaka 1,000, wenye haki watazichunguza kesi za wanadamu wale waovu pamoja na malaika wale walioanguka, akiwamo na kiongozi wao Shetani. Ni jambo lifaalo jinsi gani kwa wafia dini, washindi, na wale walio na makovu ya vita walioifuata injili kuweza kuichunguza na kuielewa ile hukumu ya Mungu aliyotoa dhidi ya waovu.

Kwa neema yake nyingi Mungu amewapa wanadamu waliokombolewa nafasi ya kutathmini alivyowashughulikia waovu. Tunaweza kuwa na maswali mengi kama haya: “mbona shangazi yangu hayupo hapa? Alionekana kana kwamba alikuwa mtu mzuri” Tutakapozipitia kumbukumbu zile na kuwahukumu wale wafu ” kulingana na matendo yao kama yalivyoandikwa katika vitabu vile” (fungu la 12), tutajionea wenyewe ya kwamba katika kushughulika kwake kote kule na wanadamu, Mungu amekuwa wa haki wala hana upendeleo kwa kila mtu. Tutaona jinsi Roho Mtakatifu alivyowapa wanadamu nafasi baada ya nafasi ili wapate kujitoa kabisa kwa Mungu, na haki ya kila hukumu itaonekana wazi.

5. Shetani Afunguliwa Mwisho Wa Ile Miaka Elfu Moja

Mwisho wa ile miaka 1,000 Biblia inatangaza hivi:
“Nikaona mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi harusi aliyepambwa tayari kukutana na mumewe” – (Ufunuo 21:2).

Mji huu wa ajabu umekuwa makao yetu kwa miaka elfu moja. Sasa Mji huu Mtakatifu – ndani yake ukiwa na Kristo na watu wote aliowakomboa – unashuka kutoka mbinguni kuja katika dunia mpya.

Je! Shetani anafanya nini mwisho wa mika hiyo 1,000?

“Wakati miaka elfu moja itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka gerezani mwake. Basi, atatoka nje, ataanza kuyapotosha mataifa yote yaliotawanyika kila mahali duniani, yaani Gogu na magogu. Shetani atawakusanya pamoja kwa ajili ya vita; nao watakuwa wengi kama mchanga wa pwani. Walipita katika nchi yote, wakaizunguka kambi ya watakatifu na mji wa Mungu aupendao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawaangamiza” – (Ufunuo 20: 7-9).

Waovu wanafufuliwa katika ufufuo wa pili mwisho wa ile miaka1,000 (fungu la 5). Wenye haki wanaposhuka duniani wakiwa ndani ya huo mji Mtakatifu, na waovu wanapofufuliwa, Shetani ata”funguliw[a] kwa muda mchache” (fungu la 3). Yeye anao tena wale waovu ili kuwaongoza na shabaha yake ni wale wenye haki. Bila kupoteza hata dakika moja, anaanza mara moja, kuwapanga waovu katika jeshi kubwa sana. Shetani anatoa amri ya kusonga mbele dhidi ya mji huo. Waovu wanapojipanga mahali pao kuuzunguka Yerusalemu Mpya (fungu la 9), mara moja wanaingiwa na hofu kuu ya kupotea – yaani kupotea milele.

6. Mandhari Ya Hukumu Ya Mwisho

hukumuHapo, kwa mara ya kwanza, wanadamu wote wanakutana pamoja ana kwa ana. Yesu anawaongoza wana wa Mungu waliokombolewa ambao wamo ndani ya mji huo. Shetani anaongoza akiwa mbele ya hilo kundi kubwa sana lililosongamana la waovu ambao wako nje ya kuta hizo. Katika wakati huu wa hatari sana, Mungu anatekeleza hatua ya mwisho ya hukumu na waovu wanapokea siku yao katika mahakama hiyo.

“Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yule aketiye juu yake. Dunia na mbingu vikatoweka mbele ya macho yake, na havikuonekana tena. Kisha nikawaona watu wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Halafu kitabu kingine, yaani kitabu cha uhai, kikafunguluwa pia. Wafu wakahukumiwa kadri ya matendo yao, kama ilivyoandikwa ndani ya vitabu hivyo” – (Ufunuo 20:11,12).

Waovu wanaposimama mbele ya hicho kiti cha enzi cha hukumu, maisha yao yote yanaonyeshwa mbele yao. Kutoka katika zile kumbukumbu zilizoko kule mbinguni, Yesu, Jaji mwenye haki, anakifunua rasmi kisa chake kamili kuhusu jinsi alivyowashughulikia wanaume, wanawake, na malaika walioanguka.

Malimwengu yote yanaangalia kwa hamu kubwa. Akisimama mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, Yesu anamwonyesha kila mmoja picha kamili ya kazi yake ya ukombozi. Anawaonyesha kwamba yeye alikuja kuwatafuta na kuwaokoa wale waliopotea. Aliingia katika dunia yetu akiwa na mwili wa kibinadamu, aliishi maisha yasiyo na dhambi katikati ya mapambano na majaribu, alitoa kafara yake ya mwisho pale msalabani, na kuhudumu kama Kuhani wetu kule mbinguni. Mwisho, Yesu anapopiga hatua kuja mbele kwa huzuni na kutamka hukumu dhidi ya wale walioendelea kwa ukaidi kuikataa neema yake, kila kiumbe katika malimwengu hayo atakiri kwamba tendo hilo la mwisho la hukumu ya Mungu ni la haki, tena ni la lazima.

“Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Imeandikwa: ‘Kama niishivyo,’ asema Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; na kila ulimi utamkiri Mungu!” – (Warumi 14:10-11).

“Kristo Yesu akawa mtii hata mauti – naam, mauti ya msalaba!. Ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, mbinguni na duniani.. kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” – (Wafilipi 2:5-11).

Tangu dhambi ilipoanza, Ibilisi amekuwa akiielezea vibaya tabia ya Mungu, akimshtaki kwamba hatendi haki. Lakini sasa maswali yote yamejibiwa, utata wote umeondolewa. Sasa kila kiumbe aliye katika hayo malimwengu anakiri kwamba Yesu, Mwana-Kondoo wa Mungu, anastahili kupewa upendo wetu na kuabudiwa.

Mpango wote na kusudi la Mungu sasa vimefunuliwa kikamilifu, na tabia ya Mungu inasimama ikiwa imethibitishwa kuwa ni ya haki.

Si wale tu waliokombolewa, bali pia wale malaika waovu pamoja na Shetani mwenyewe watakiri kwamba njia ya Shetani imekuwa na makosa na ya kwamba njia za Mungu ni za haki na za kweli. Wote wanaona wazi kwamba uovu na uchoyo vimeleta huzuni tu na kutokuridhika, na kwamba mambo hayo hayafai kuendelea.

7. Dhambi Yaufikia Mwisho Wake

Ingawa Shetani na kundi lile kubwa sana lililosongamana la watu wale waovu wanakiri kwamba njia ya Mungu haijabadilika, tabia zao bado zina dhambi. Na baada ya hukumu ile kutamkwa wale waovu:
“Wakatembea kijeshi kupitia katika mapana ya nchi, wakaizingira kambi ya watu wa Mungu, mji ule aupendao. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza kabisa. Na yule Ibilisi, aliyekuwa, anawapotosha katupwa ndani ya ziwa linalowaka moto wa kiberiti…. Kisha kifo na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili la moto ndicho kifo cha pili. Mtu ye yote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika kitabu kile cha uhai, alitupwa katika ziwa la moto” – (Ufunuo 20:9-15).

Katika hukumu ya mwisho moto wa milele wa Mungu utateketeza dhambi pamoja na wale ambao kwa ukaidi wao wanaing’ang’ania. Shetani na wote waliopotea wanaangamia katika hicho “kifo cha pili,” yaani, wanapatikana na kifo cha milele ambacho katika hicho hawataamshwa kamwe. Mwenendo wao wa uasi umewaacha waovu hao wakiwa hawafai kuingia katika furaha ya kweli, kisha wanateketezwa pamoja na Ibilisi na malaika zake. Moto ule utokao mbinguni unaitakasa dunia kabisa kutokana na uharibifu wa dhambi; hatimaye Mungu anakuwa na ulimwengu safi, usioweza tena kutiwa makovu ya uovu. Pambano hilo la kishujaa kati ya wema na uovu, kati ya Kristo na Shetani, sasa limekoma, na Kristo anatawala. Pazia linayafunika matokeo ya dhambi ya zamani yaliyofuatia, kasha linafunuliwa ili kuuonyesha ulimwengu mpya wenye utukufu usiokuwa na kikomo.

8. Dunia Inatakaswa Na Yafanywa Upya

Kutoka katika majivu yale ya maangamizi makuu ya mwisho, Mungu ataiumba dunia mpya:
“Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita… Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu.. “Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye fanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao. Naye atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, hayatakuwapo tena kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita… Tazama, nayafanya yote kuwa mapya” – (Ufunuo 21:1-5).

Itakapokuwa imerudishwa katika uzuri wake wa awali, dunia hii itakuwa makao ya waliokombolewa milele hata milele. Ikiisha kukombolewa mbali na choyo, magonjwa, na maumivu, tutayachunguza na malimwengu yote na tutakuwa na uhusiano wa ajabu na kuukuza, na umilele wa kuketi miguuni pake Yesu na kusikiliza, kujifunza, na kupenda. (Kwa maelezo kamili ya dunia mpya, ukipenda waweza kusoma tena Somo la 9.)

Je! wewe unapanga kuwa wapi siku hiyo? Je! umeamua kuwa pamoja na Kristo ndani ya mji ule na kuokolewa milele? Au utakuwa nje ya ule mji bila Kristo na kupotea milele?

Kama wewe umeyakabidhi maisha yako mikononi mwake Yesu, basi, huna haja ya kuionja ile hofu isiyoneneka ya wale walio nje ya mji ambao wanatambua kwamba wamepotea milele. Haidhuru maisha yakuletee kitu gani, kama wewe unayaweka maisha yako mikononi mwake Yesu hivi sasa, basi, unaweza kuwa ndani ya mji ule pamoja na Kristo na pamoja na wale waliokombolewa. Endapo wewe hujafanya hivyo, basi mpe Yesu moyo wako sasa, naye atakuzungushia upendo wake na msamaha. Hii ni nafasi yako ya pekee. Hii ndiyo siku yako ya wokovu kwako.

© 2004 The Voice of Prophecy