Yachunguzeni Maandiko Somo la 07 – Siku Ya Bwana

Mamilioni ya Wakristo huenda kanisani kila Jumapili, siku ya kwanza ya juma. Wanafanya hivyo wakiamini kuwa hiyo ndiyo siku ambayo Mungu aliitenga na kuibariki kwa ajili ya kumwabudu. Baadhi yao wanajua kuwa siku aliyoitenga Mungu kwa ajili ya mambo matakatifu ni Jumamosi, siku ya saba ya juma, lakini wanaamini kuwa, mahali fulani huenda kuna mtu aliyeibadilisha siku hiyo kutoka Jumamosi kwenda Jumapili. Ni kweli kwamba kuna badiliko lilifanyika. Lakini swali hasa ni kwa mamlaka ya nani?

Kama Mungu alibadili mawazo kuhusu siku yake maalum ya kupumzika, siku aliyoiweka kama kumbukumbu ya kuumbwa kwa dunia, bila shaka atakuwa ametuagiza katika Maandiko Matakatifu juu ya jambo hilo. Hebu sasa tuigeukie Barua ya Mungu, yaani Biblia, ili tuone anasema nini kuhusu siku yake.

1. Je, kuna siku ambayo Mungu anaiita kuwa ni yake?

“Nalikuwa katika Roho, Siku ya Bwana.” Ufu. 1:10. “Kama ukigeuza mguu wako usiihalifu Sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita Sabato siku ya furaha, na Siku Takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe, ndipo utakapojifurahisha katika BWANA.” Isa. 58:13,14.

2. Je, Yesu Kristo ni Bwana wa siku ipi?

“Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.” Mt. 12:8.

Jambo hili ni wazi – Yesu mwenyewe anatamka wazi kuwa yeye ni Bwana wa Sabato. Siku zote amezifanya yeye, lakini siku ya saba ameifanya kuwa yake.

3. Kuna sababu yo yote iliyomfanya Mungu aichague Siku ya Saba na siyo zile nyingine?

“Maana, kwa siku sita BWANA alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo BWANA akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” Kut. 20:11. “Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.” Mwa. 2:2,3. “Tena naliwapa Sabato zangu, ziwe ishara kati ya mimi na wao, wapate kujua ya kuwa mimi, BWANA, ndimi niwatakasaye.” “Zitakaseni Sabato zangu; zitakuwa ishara kati ya mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.” Eze. 20:12,20.

Siku ya saba ni kumbukumbu ya tukio maalum. Kuzaliwa kwa dunia na vyote vilivyomo. Mungu aliiweka ili tuendelee kumkumbuka yeye kama Muumbaji. Na kuwa ndiye anayetutakasa.

4. Kama Yesu ndiye Bwana wa Sabato, Yeye mwenyewe alikuwa na desturi gani kila siku ya Sabato?

“Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya Sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome.” Luka 4:16.

Biblia iko wazi hapa! Ilikuwa ni desturi ya Yesu kwenda kanisani kila siku ya Sabato. Desturi siyo tukio la mara moja au mbili tu.

5. Lakini ninaweza kuijua namna gani siku ya saba?

Ni rahisi sana. Sote tunajua kuwa Yesu alikufa siku ya Ijumaa. Na kwa sababu hiyo dunia nzima huadhimisha siku ya Ijumaa Kuu kukumbuka kifo cha Yesu kwa kuwa Yesu alikufa Ijumaa. Sasa tuangalie siku ambayo Yesu alikufa inaitwaje.

“Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na Sabato ikaanza kuingia.” Luka 23:54.

Siku hiyo ya Ijumaa ilikuwa ya Maandalio na siku iliyofuata ilikuwa ni Sabato – siku inayofuata baada ya Ijumaa ni Jumamosi.

Zaidi ya hayo, sote tunajua kuwa dunia nzima huadhimisha Jumapili ya Pasaka kukumbuka kufufuka kwa Yesu kwa kuwa Yesu alifufuka Jumapili. Hebu tuangalie siku aliyofufuka Yesu inaitwaje katika Biblia. “Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari. Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi.” Luka 24:1,2.

Inaitwa Siku ya Kwanza. Jumapili ni siku ya kwanza na ukihesabu kuanzia Jumapili, siku ya kwanza, siku ya saba itakuwa Jumamosi.

Zaidi ya hayo, angalia Marko Mtakatifu anavyoelezea:

“Hata Sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome wainunua manukato wapate kwenda kumpaka. Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza.” Marko 16:1,2.

Sabato ilipokwisha ndipo ikafuata siku ya kwanza, yaani Jumapili ambayo Yesu alifufuka. Siku ya Sabato ni ile iliyo kabla ya siku ambayo Yesu alifufuka, yaani, kabla ya Jumapili. Hiyo ni Jumamosi. Kwa muhtasari, Sabato ni siku iliyo katikati ya Ijumaa (siku aliyokufa Yesu) na Jumapili (siku aliyofufuka).

6. Lakini nimesikia mchungaji wangu akisema kuwa Yesu aliifuta Sabato.

“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Maka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.” Mt. 5:17-19.

Yesu anakataa! Hakuja kufanya kazi hiyo. Mungu mwenyewe anasema hawezi kufanya hivyo!

“Mimi sitalihalifu agano langu, sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.” Zab. 89:34. “Kwa kuwa mimi, BWANA, sina kigeugeu.” Mal. 3:6.

7. Pengine badiliko hilo lilifanywa na Mitume?

“Na kutoka hapo tukafka Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha. Hata siku ya Sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.” Mdo. 16:12,13.

Hapana. Mitume wasingeweza kufanya jambo lo lote kinyume na Bwana wao! Siku ya Sabato walikuwa wakienda kusali.

8. Una maana hata Paulo alikuwa anakwenda kanisani Siku ya Sabato?

“Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya Maandiko Sabato tatu.” Mdo. 17:2.

9. Siyo kwamba Sabato iliwahusu Wayahudi peke yao?

“Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya Sabato ya pili.” “Hata Sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie Neno la Mungu.” Mdo. 13:42,44. “Akatoa hoja zake katika sinagogi kila Sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.” Mdo. 18:4.

10. Kama Mungu mwenyewe alipumzika Siku ya Sabato, Yesu mwenyewe alikuwa na desturi ya kwenda kanisani siku ya Sabato na Mitume pia, sasa imekuwaje leo sehemu kubwa ya Wakristo wana desturi ya kwenda kanisani Jumapili?

“Akawaambia, Isaya alitabiri vema juu yenu ninyi wanafki, kama ilivyoandikwa, Watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami; nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu. Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Akawaambia, Vema! Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu.” Mk. 7:6-9.

Hayo ni mapokeo ya wanadamu.

11. Je, Mungu alijua kuwa kuna taasisi inayompinga ambayo ingejaribu kufanya badiliko hilo?

“Naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati.” Dan. 7:25.

Taasisi hii ingediriki kubadili majira (muda) aliyopanga Mungu pamoja na Sheria zake. Zingatia kuwa “atanena maneno kinyume chake Aliye juu.”

12. Taasisi hii iliwezaje kufanya jambo hili la kukufuru namna hii?

Historia inatueleza kuwa mnamo mwaka 321 B.K. Mfalme Konstantino wa Dola ya Kirumi alitoa agizo lililotaka mahakama zote, wakazi wote wa mijini pamoja na wataalam wote wapumzike katika “siku ya kuheshimika ya jua.”

Konstantino pamoja na Warumi wenzie walikuwa waumini wa dini ya kipagani iliyokuwa ikiabudu jua. Warumi wengi hawakutaka kuachana na ibada yao ya jua hata baada ya kuwa Wakristo. Hivyo baada ya muda Viongozi wa kanisa kule Rumi, walianza kukubaliana na upagani na hatimaye walianza kuiita Jumapili kuwa ni Siku ya Bwana. Katika Baraza la Laodikia, Kanisa la kule Rumi lililokuwa limekubali kuingiza upagani katika Ukristo, lilitoa agizo lifuatalo mnamo mwaka 364 B.K.:
“Wakristo wasifanye mambo ya Kiyahudi na kukaa bila kazi siku ya Jumamosi, bali watafanya kazi katika siku hiyo; lakini siku ya Bwana (Jumapili) wataiheshimu kwa namna ya pekee na wakiwa kama Wakristo, ikiwezekana, wasifanye kazi siku hiyo. Kama wakipatikana wanafanya mambo ya Kiyahudi, watakatiliwa mbali na Kristo.”

Hivyo Wakristo wengi wakaanza kugeukia Jumapili kutokana na maagizo hayo yaliyotokana na chuki kwa Wayahudi.

13. Je, Biblia iliwahi kutabiri kuwa watu wangeligeukia jua huku wakijifanya kumwabudu Mungu?

“Akanileta mpaka ua wa ndani wa nyumba ya BWANA, na tazama, mlangoni pa hekalu la BWANA, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, wamelipa kisogo hekalu la BWANA, na nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki.” Eze. 8:16. “Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharaibifu, yule mpimgamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” 2 Thes. 2:3,4. Unabii huu uko wazi na umetimia. Watu wengi leo wanaitwa Wakristo lakini wamechagua siku ya jua kwa ajili ya kumwabudu Mungu.

14. Inawezekana kweli watu wote hawa wawe wamedanganyika?

“Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba ; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.” Mt. 7:13,14,21-23.

Wanaoiona njia nyembamba iendayo uzimani ni wachache. Kumwita, Bwana, Bwana, au kulitaja jina lake haitoshi! Kinachotakiwa ni kuyafanya mapenzi yake.

15. Je, hii Sabato itaendelea kushikwa hadi lini?

“Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya, zitakavyokaa mbele zangu, asema BWANA, ndivyo uzao wenu na jina lenu litakavyokaa. Na itakuwa mwezi mpya hata mwezi mpya, na Sabato hata Sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema BWANA.” Isa. 66:22,23.

Watu wote wataendelea kuhudhuria mbele za Mungu na kumwabudu kila Sabato, hata katika mbingu na nchi mpya ambazo Bwana atazifanya! Yesu amekuwa wazi sana juu ya jambo hili kwamba hakuja duniani kubadili amri za Baba yake. Alikuja kubadili mioyo ya wanadamu ili wamgeukie Mungu na kufanyika watoto wake. “Wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu” (Yn. 1:12). Wewe pia unaweza kufanyika mtoto wa Mungu kama ukiwa tayari kumpokea Yesu na kuyafanya mapenzi ya Baba yake aliye mbinguni.

Je, uko tayari sasa kumpokea Yesu ili uwe mmoja kati ya wale wachache wanaoiona njia nyembamba iendayo uzimani?