Yachunguzeni Maandiko Somo la 12 – Kanisa La Kweli

Hivi karibuni nilimsikia mtu akilalamika, “Nimejaribu kila njia kulitafuta Kanisa la Mungu, lakini nimekata tamaa. Kuna mamia ya madhehebu na vikundi vya dini hapa duniani. Mengi yanadai kuwa ndiyo kanisa la kweli la Mungu, na yote yanafanana katika mambo fulani, lakini yanatofautiana katika mengine. Hata kama nikitumia maisha yangu yote kuchunguza mafundisho ya makundi haya yote sitafanikiwa. Nimechanganyikiwa! Najisikia kama vile Mungu ananichezea. Juhudi zangu zote zinakuwa bure na hazina maana.” Kwa bahati mbaya mamilioni wana hisia kama hizo. Pengine hata wewe unajisikia hivyo.

Je, unajua kwamba katika Ufunuo Mungu anaelezea wazi kabisa Kanisa lake la siku hizi za mwisho linavyopaswa kuwa, na, kama ukijua anavyosema, unaweza kulitambua Kanisa lake la kweli kwa urahisi kabisa kati ya yote kama vile unavyoweza kuitambua bendera ya Taifa lako kati ya bendera zingine zote?

Ndiyo maana Shetani huchanganyikiwa anapoona watu wanaanza kukisoma kitabu cha Ufunuo. Anajua kuwa Kanisa la Mungu limeelezewa katika kitabu hicho, naye hutumia kila mbinu kutufanya tusikisome kwa makini. Kama kila mtu angesoma na kukielewa kitabu cha Ufunuo, Ufalme wa Shetani ungeingia katika hatari kubwa, na jina kuu la Mungu pamoja na Kanisa lake lingeinuliwa kwa namna ya ajabu.

Hebu tuone jinsi kitabu cha Ufunuo kinavyolielezea Kanisa la Mungu. Maelezo hayo yako katika Sura ya 12. Ikiwezekana soma sura yote ya 12 kabla ya kuanza somo hili.

1. Yesu alisema kuwa siku za mwisho zitakuwa kama zilivyokuwa siku za Nuhu (Luka 17:26). Je, kulikuwa na njia ngapi za kuokoka wakati wa Nuhu?

“Bwana akamwambia Nuhu, Ingia wewe na jamaa yako yote katika safna maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu.” Mwa. 7:1.

2. Biblia inasema Yesu anazo Imani au Madhehebu mangapi?

“Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.” Efe. 4:5.

Kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu, Mungu anayo safna au kanisa moja tu linalokwenda kwenye usalama. Hakikisha kwamba umepanda safna ya kweli.

3. Bila shaka wapo Wakristo waaminifu katika makanisa yote. Lakini kwa kuwa Mungu ana Kanisa moja tu, Wakristo waaminifu, walio kwenye makanisa mengine watakwenda wapi?

“Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na Mchungaji mmoja.” “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.” Yn 10:16,27.

Yesu anaelezewa hapa kama Mchungaji Mwema, watu wake ni kama kondoo, na kanisa lake ni kama zizi. Yesu anasema wazi kuwa baadhi ya kondoo wake bado hawamo katika Kanisa lake, lakini atawaita, nao watamfuata kwenye Kanisa lake.

Ishara za Kanisa la Mungu

4. Je, Mungu analielezea Kanisa lake kwa ishara gani katika unabii?

“Nikusawazishe na nini nipate kukufariji, Ee bikira binti Sayuni?” Omb. 2:13. “Na kuuambia Sayuni, ninyi ni watu wangu.” Isa. 51:16.

Mara kwa mara Biblia hulifananisha Kanisa la Mungu na mwanamke safi au bikira.

5. Katika Ufu. 12:1 Yesu analielezea Kanisa lake kwa ishara ya mwanamke saf. Mwanamke huyu amevikwa nini?

Amesimama juu ya nini na kichwani kwake kuna nini? “Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili.” Ufu. 12:1.

Amevikwa jua, amesimama juu ya mwezi na kichwani ana taji yenye nyota kumi na mbili. Zingatia:

(a) JUA linamwakilisha Yesu pamoja na haki yake “kwa kuwa Bwana Mungu ni jua na ngao.” Zab. 84:11.

(b) MWEZI hauna nuru yake wenyewe, huakisi nuru toka juani.

Mwezi huwakilisha Injili kwa mifano katika Agano la Kale. “Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.” Ebr. 10:1.

(c) Taji ya nyota 12 inawakilisha kazi ya Mitume Kumi na Wawili iliyong’aa miaka ya mwanzo wa Kanisa.

Zingatia: Kwa kuwa jua na mwezi vinafanya kitu kizima, (yaani, usiku na mchana), Ishara hizi zinawakilisha historia ya kanisa katika ujumbe wake. Yaani kanisa kabla ya msalaba na kanisa baada ya msalaba.

6. Je, jambo gani kubwa lililotokea katika Kanisa la Mungu?

“Naye alikuwa ana mimba, akilia, hali ana utungu na kuumwa katika kuzaa.” “Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fmbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi.” Ufu. 12:2,5.

Mtoto wa kiume alizaliwa, kisha akanyakuliwa hadi kwenye kiti cha enzi.

7. Mtoto huyu ni nani ambaye alipaa kwenda mbinguni na atawatawala Mataifa?

“Jina lake aitwa, Neno la Mungu… Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige Mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fmbo ya chuma.” Ufu. 19:13-15.

8. Je, ni jambo gani lilimkabili yule mwanamke, yaani Kanisa la Mungu?

“Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba. Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.” Ufu. 12:3,4.

Joka alikuwa anasubiri kumla mtoto wake mara baada ya kuzaliwa.

9. Joka huyu ni nani?

“Kulikuwa na vita mbinguni … Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote, akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.” Ufu. 12:7-9.

Ibilisi ndiye Joka, ambaye ambaye kwa kumtumia Mfalme Herode aliua watoto wadogo wote kule Bethlehemu katika jaribio la kutaka kumwua Yesu mara baada ya kuzaliwa.

10. Baada ya kushindwa kumwangamiza Yesu alipokuwa hapa duniani, Shetani akaamua kufanya nini?

“Na yule joka alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.” Ufu. 12:13.

Aliamua kumwudhi mwanamke, yaani, Kanisa la Mungu.

11. Je, Kanisa la Mungu lilifanya nini kutokana na mateso hayo?

“Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambapo ana mahali palipotengenezwa na Mungu, ili wamlishe huko kwa muda wa siku elfu na mia mbili na sitini.” Ufu. 12:6.

Kanisa la Mungu likajifcha kwa muda wa siku 1260. Siku 1 ya unabii ni sawa na mwaka 1 (Eze. 4:6).

Hivyo Kanisa la Mungu likajifcha katika mapango na nchi zisizokaliwa na watu kwa miaka 1260.

Historia inaeleza wazi kwamba Mamlaka ya Papa ndiyo iliyotesa Kanisa la Mungu kwa miaka 1260. Tangu mwaka 538 B.K. Mamlaka ya Papa iliposhika hatamu katika Ukristo kutokana na barua ya mfalme wa Roma, Justinian, iliyomtambua Askofu wa Roma kama mkuu wa makanisa yote. Kipindi hiki kiliishia mwaka 1798 wakati Jemadari wa Kifaransa, Berthier, alipoingia Roma na kumteka nyara Papa. Kwa uchache, Wakristo milioni 50 waliuawa kwa ajili ya imani yao katika kipindi hiki cha mateso.

Kanisa la Mungu Lililosalia Katika Siku za Mwisho.

Hebu angalia ishara hizi katika Ufu. 12:17; Ufu. 12:7.

A. Joka – tumekwisha kuona kuwa ni Ibilisi.

B. Mwanamke – tumekwisha kuona kuwa ni Kanisa la Kweli la Mungu.

C. Waliosalia – Waliobaki katika siku za mwisho. Baada ya mateso.

D. Amri za Mungu – Amri Kumi.

E. Ushuhuda wa Yesu – “Ushuhuda wa Yesu ni Roho ya Unabii” (Ufu. 19:10).

Hebu tuliandike tena fungu la 17 katika lugha ya leo. “Shetani akalikasirikia Kanisa, akaenda kupigana na Kanisa la Mungu lililosalia katika siku za mwisho, ambalo linashika Amri Kumi za Mungu na kuwa na Roho ya Unabii.”

12. Kuna sifa gani muhimu za Kanisa la Mungu zinazotajwa katika Ufu. 12:17?

A. Washikao Amri za Mungu.

B. Wana Roho (Karama) ya Unabii.

Kwa hiyo, Kanisa la Mungu katika siku hizi za mwisho ni lile lenye Karama ya Unabii, na linaloshika Amri zote za Mungu, pamoja na Sabato ya Siku ya Saba kama inavyoagizwa katika Amri ya Nne (Kut. 20:8- 11). Yesu bado anatuambia, “Mkinipenda, mtazishika amri zangu” (Yn 14:15; 1 Yoh. 5:3). Haiwezekani kuwa tunampenda kweli bila kuzishika amri zake.

Wapo Wakristo wengi wenye upendo katika makanisa yasiyoshika Sabato au kuwa na Karama ya Unabii. Hata hivyo, katika makanisa hayo hakuna linaloweza kuwa Kanisa la Mungu la siku za mwisho, ambalo Yesu anawaita watu wake wote waingie, kwani Kanisa lake ni lazima liwe na sifa zote mbili.

Injili ya milele ambayo Kanisa la Mungu ni lazima liihubiri kwa nguvu katika siku hizi za mwisho, ni pamoja na mambo matatu ya pekee ambayo Yesu mwenyewe ameagiza. Ujumbe huu ni lazima uhubiriwe kwa dunia nzima (Ufu. 14:6; Mt. 24:14). Je, ujumbe huu ni upi?

“[Malaika wa kwanza] akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.” “Malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha Mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.” “Malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake… atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu” Ufu. 14:7,8,9,10.

Kanisa la Mungu litafundisha kwamba tuko katika kipindi cha saa ya hukumu kabla ya kurudi kwa Yesu, na kwamba ni lazima tumwabudu Mungu kwa kushika Sabato ambayo ni ishara ya uwezo wake wa kuumba.

Je, inawezekana uko katika Babeli? Kanisa la Mungu la siku za mwisho lazima lipige mbiu ya kuwaita watu watoke Babeli (Ufu. 18:4) – (Babeli ni machafuko, yaani mafundisho yasiyo na msingi wa Biblia).

Kanisa la Mungu ni lazima pia liwatahadharishe watu dhidi ya kumsujudia mnyama na kuipokea alama yake.

13. Ni mambo gani mengine ambayo Kanisa la Kweli la Mungu litasisitiza?

“Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” Ufu. 12:11.

Kanisa la kweli litafundisha wazi kuwa wokovu na haki ni kwa imani katika Yesu Kristo peke yake. “Hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo kuokolewa kwalo.” Mdo. 4:12.

14. Je, mtu anapolitambua Kanisa la Mungu, ni lazima kujiunga nalo?

“Bwana akalizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa.” Mdo. 2:47.

Waliokuwa wanaokolewa walikuwa wakizidishwa katika Kanisa la Mungu.

Leo hii ni muhimu kuingia katika Safna au Kanisa la Mungu kama ilivyokuwa muhimu kuingia katika Safna wakati wa Nuhu. Kumbuka kwamba Yesu anakusudia kuliokoa Kanisa.

“Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafsha kwa maji katika Neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.” Efe. 5:25-27.

Kulingana na Biblia ni lazima tulitafute Kanisa ambalo:

A. linashika amri zote ikiwemo ya nne inayoagiza kushika Sabato;

B. ni la Kikristo kwa kuwa linashika imani ya Yesu;

C. lina Karama ya Unabii, na

D. linatangaza Ujumbe wa Malaika Watatu wa Ufunuo 14:6-12.

15. Je, ni makanisa mangapi yanayotimiza sifa za Kanisa la Mungu kama zilizotajwa hapo juu?

“Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.” Efe. 4:5.

Lipo kanisa moja tu! Kanisa ambalo limekuletea ujumbe huu linazo sifa zote hizi.

Inawezekana umekuwa ukifuata imani za ukoo, wazazi, kanisa fulani au mafundisho ya mtu fulani maarufu. Je, utaamua sasa kuisikia sauti ya Yesu na kumfuata kama asemavyo katika Neno lake?

Sikia anavyosema:

“Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.” Yn 10:27.

Umeisikia sauti yake. Je, utamfuata sasa na kujiunga na Kanisa lake